Matendo ya Sheria na Imani

 

Matendo ya Sheria na Imani




LAZIMA tutambue kwamba, tuna vitu viwili tofauti ambavyo lazima tuviweke katika sehemu mbili tofauti. “Matendo ya sheria” ni sehemu ya kwanza ya maisha ya mwanadamu, na “Imani” ni sehemu ya pili yake mwanadamu yeyote anayemwamini Kristo. Na ni lazima pia tuelewe maana sahihi za matendo ya sheria na imani.

Kila mwanadamu ambaye ni wa uzao wa Adamu, amewahi kuwa chini ya sheria na hiyo inamaanisha kwamba amewahi kuwa wa matendo ya sheria. Hapa haijarishi kama ni Myahudi au ni Mmataifa, au kama ni Msabato au ni Mjumapili. Wanadamu wote wamewahi kuwa chini ya sheria, hata Yesu Mwenyewe alipozaliwa na mwanadamu tu akawa chini ya sheria: “Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, AMEZALIWA CHINI YA SHERIA, 5 kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.” (Gal. 4:4,5).

Inashangaza kuwa Kristo alizaliwa chini ya sheria ili auone ugumu uliopo kwetu na ajifunze kwamba ni “wapi sisi tunashindwa” ili apate kutusaidia kikamilifu kushinda (Waebrania 2:18). Njia pekee ya kutusaidia, ni lazima Yesu pia angeonja hali yetu wenyewe na udhaifu wetu wenyewe wa kuwa chini ya sheria, ili apate kutuondoa chini ya sheria: “Hivyo ilimpasa [Yesu] kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake.” (Waebrania 2:17, pia 4:15). Yesu alikuja kuwaokoa walio chini ya sheria. Jinsi gani swala hili liko wazi kwamba walio chini ya sheria ni wanadamu wote na si Wayahudi, wala Wasabato!

Ukweli huu umefundishwa na Paulo mwenyewe anapoonyesha kwamba kuwa “chini ya sheria” ni vilevile kama kuwa “chini ya dhambi”, harafu anahitimisha kwamba: “Kwa maana tumekwisha kuwashitaki Wayahudi na Wayunani ya kwamba pia wamekuwa chini ya dhambi;” (Rum. 3:9), kitu ambacho hakikataliki kwamba Wayahudi na Wamataifa, Wasabato na Wajumapili, kabla ya kumjua Kristo wote walikuwa chini ya sheria. Paulo anaendelea kuonyesha maana ya wanadamu wote kuwa chini ya sheria na dhambi na kusema kwamba: “kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. 11 Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu.
12 Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.
13 Koo lao ni kaburi wazi, Kwa ndimi zao wametumia hila. Sumu ya fira i chini ya midomo yao.
14 Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.
15 Miguu yao ina mbio kumwaga damu.
16 Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao.
17 Wala njia ya amani hawakuijua.
18 Kumcha Mungu hakupo machoni pao.” (Rumi. 3:10-18).

HIVYO Paulo, akiwemo na yeye mwenyewe (angalia Rum 3:7), haachi hata mwanadamu mmoja kuwa na haki, bali anaonyesha kwamba wote Wayahudi na Wamataifa wako chini ya sheria na chini ya dhambi, tena hatimaye anahitimisha kwamba: “Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu;” (Rum. 3:19). Ndipo inakuwa wazi kwamba, wanadamu wote wako chini ya sheria, na sheria ina nena kwa ajili yao ili kila mwanadamu asijigambe, na ulimwengu wote; yaani, kila mwanadamu (Myahudi au Mmataifa) awe chini ya hukumu ya Mungu kwa sababu hatii torati (angalia Rum. 2:13) na hiyo ndiyo sababu kila kinywa cha mwanadamu kimezimishwa na kufumbwa kabisa kwa kuwa hana uwezo wa kutii sheria na sheria ndicho kiPImo cha utii ambacho Mungu atakitumia kumuhukumu kuwa na hatia.

Paulo anaongezea kwamba: “kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; 24 wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu;” (Rum. 3:23,24). Hili linawahusu uzao wa Adamu wote. Wanadamu wote, Wayahudi kwa Wamataifa, wako chini ya sheria na dhambi, na kwa vyovyote hawawezi kuokolewa; kwani pia wako chini ya hukumu vilevile. Tumaini lao wote ni kumwamini Yesu. Hivyo turudi kwenye maada na kujifunza zaidi.
\
MATENDO YA SHERIA NA IMANI.
/
Sasa swali la mhimu ni kwamba. Je! Mtu gani ni wa matendo ya sheria na mtu gani ni wa imani? Tumejifunza hapo juu kwamba wanadamu wote wako chini ya sheria na dhambi. Maandiko yamewafunga wote chini ya sheria na dhambi, ili kusudi wale wanaoamini wahesabiwe haki. Pia ni lazima tujue kuwa wote walio chini ya sheria ni wale waliozaliwa kwa mwili tu (wana wa Adamu wa zamani), hao ndio wa matendo ya sheria, hujitahidi na kujilazimisha kutenda tendo jema, na haki yao huhesabiwa kwa matendo yao. Lakini kwa kuwa matendo yao si kamilifu, hivyo wako chini ya dhambi na hukumu daima; na Paulo anasema juu yao kwamba: “maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye.” (Gal. 3:10). Wanapenda kumpendeza Mungu, lakini hawawezi kwa sababu wao ni uzao wa mwili (uzao wa kwanza), na yote wanayojitahidi kufanya yanakuwa ni bure na hasara, tena kibaya zaidi yanakuwa ni deni (Rum. 4:4).

Akiongelea udhaifu wao, Paulo anasema: “mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.” (Gal. 5:17). Mwili hutamani kuvunja sheria, lakini roho hutamani kutii sheria; “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu;” (Yn. 6:63) Anasema Yesu “roho i radhi lakini, mwili ni dhaifu” (Mt. 26:41). Mwili ni dhaifu katika kutii sheria, lakini una nguvu katika kuvunja sheria; hivyo mtu ambaye amezaliwa kwa mwili tu, mwili wake humwendesha kutenda dhambi; hata kama akijitahidi vipi kufanya matendo ya sheria, kamwe hawezi; kwa sababu hafanyi kwa uhuru, bali kana kwamba ni kwa kujilazimisha kitu kinachompelekea kumchukia Mungu, na kuona kuwa ni mzigo usioweza kubebeka. Mtu kama huyo, awe Myahudi au Mmataifa, yuko chini ya sheria na chini ya dhambi na hukumu.

Wengine wanaweza kuuliza kuwa, Je! Inawezekanaje mtu ambaye hajawahi hata kusoma sheria aijue sheria? Kila mtu aliyezaliwa na mwanadamu anapokua kufikia umri wa kutambua mema na mabaya, tayari hutambua sheria ya Mungu (haijarishi kama hatambui baadhi), lakini anatambua kabisa kwamba kuiba, kuzini, kuua, kuloga, kusema uongo, kudhurumu, kutamani, kuonea, n.k ni makosa mbele za Mungu. Na daima huishi akijitahidi na kujilazimisha ili ayaache mambo hayo na kumpendeza Mungu, lakini hawezi kwa sababu yuko katika mwili (uzao wa kwanza); mwili humwendesha kufanya yale ambayo alitakiwa asiyafanye. Pia inawezekana kabisa mtu awe amebatizwa ubatizo wa maji mengi, lakini awe bado yuko katika mwili, kwa sababu ya upungufu wa imani. Aidha alibatizwa bila kuamini, au aliamini ndio, lakini baadaye akaingiza mashaka, bali imeandikwa “mwenye haki ataishi kwa imani” (Rum. 1:17), kwa maneno mengine “mtu anayetaka kutenda haki au kutenda sheria, lazima aamini daima”; kwa sababu ni kupitia imani ndipo anapewa uwezo wa kutunza sheria na kuwa mwenye haki.

IMANI HUTENDAJE KAZI KULIKO MATENDO YA SHERIA?
_
Tunaambiwa na Paulo kwamba: “Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo.” (Gal. 5:6), “Imani itendayo kazi kwa upendo” ni nini? Akifafanua swala hili, Paulo anasema: “kutahiriwa kwafaa kama ukiwa mtendaji wa sheria, lakini ukiwa mvunjaji wa sheria kutahiriwa kwako kumekuwa kutokutahiriwa.” (Rum 2:25). Imani itendayo kazi kwa upendo ni yale matendo mema yanayofanywa na mkristo mwenye imani kwa uhuru na upendo bila chuki wala vikwazo moyoni. Huitii sheria kwa furaha na kupenda kana kwamba kwake hakuna sheria (Gal. 5:22,23). Hii ni kinyume na mtu wa matendo ya sheria, mtu wa matendo ya sheria hujitahidi kutii sheria lakini bila upendo, bali huku akiichukia na kukwazika moyoni. Akitamani kwamba ni heri sheria ingekuwa haipo; kwake huyo hufanya sheria kana kwamba ipo, lakini mtu wa imani hufanya sheria kana kwamba haipo, na hata kama ingekuwa haipo kweli bado angefanya inayoyaagiza; kwa kuwa yeye ndivyo alivyo, tofauti na mtu wa matendo ambaye hujaribu kufanya sheria wakati yeye yuko kinyume na sheria na ugumu ukimzidia huichukia sheria.

KWANINI SWALA HILI HUWA?: Kwa sababu mtu anayeamini huzaliwa upya kwa Roho; hupewa Roho Mtakatifu ndani yake, Roho Mtakatifu humfanya mtu achukie kila kitu ambacho ni kibaya mbele za Mungu. Mtu mwenye Roho Mtakatifu huwa mtu wa kiroho, na hufanana kabisa na sheria ambayo nayo ni ya kiroho (Rum. 7:14). Uadui kati yake na sheria unakuwa umeondolewa (Efe. 2:15; Kol. 2:14). Anakuwa anafanya sheria kama kitu anachokipenda kukifanya, wala si kwa kujilazimisha tena kama alivyo mtu wa kimwili, ambaye hajazaliwa upya na hana Roho Mtakatifu. Hii ndiyo haki inayopatikana kwa imani, na inaitwa haki ya Kristo; kwa sababu ni neema ya Mungu kwamba wewe uzaliwe upya na Roho akae ndani yako ufananishwe na sheria ya Mungu, ili tena usipate ugumu wa kuona kwamba unafanya mzigo, bali uwe na furaha kwamba unafanya sheria ambayo ni furaha yako mwenyewe, ni kitu unachokipenda, na ndio maana sheria kubwa ni “upendo”; torati yote imetimilika hapo, kama mtu anaweza kufanya yote kwa kutaka na kupenda, basi sheria kuu ni upendo, maana upendo ndio unaombidisha mtu kuifanya torati bila kukwazika. Lakini upendo hauji bila imani, na upendo ndiyo Roho Mtakatifu; ambaye hawezi kuingia kwenye roho ya mtu asiyeamini. Haijarishi mtu ana dhambi kiasi gani au amechafuka vipi, lakini akiamini tu kwa moyo, Roho Mtakatifu saa hiyohiyo anakaa ndani yake. (soma Matendo 10:44-48); ambapo watu waliomwamini Yesu walipokea Roho kabla hata hawajabatizwa kwa maji.

Mtu wa kimwili, ni mtu yeyote ambaye amezaliwa na mwanadamu, lakini hana imani ya Kristo na hajazaliwa kwa Roho. Huyo hawezi kutii sheria ya Mungu hata ajilazimishe vipi: “Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu wala haiwezi kutii” (Rum 8:7). Mtu wa kimwili daima yuko chini ya sheria na dhambi na hukumu, hapaswi kujisumbua kutii sheria badala yake anapaswa kumwamini Yesu. Sheria inamuongoza kumwamini Yesu. Paulo anasema: “Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa.” (Gal. 3:23). Wanadamu wote, kabla ya kumwamini Yesu wako chini ya sheria, lakini mtu anapomwamini Yesu sasa wakati huo ndio anatoka chini ya sheria na kuwa chini ya neema. Paulo anaendelea kusema: “Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani.” (Gal. 3:24). Wakati mtu wa kimwili anapoona kuwa ameshindwa kuitii torati, ndipo anajiona hana nguvu za kushinda yeye mwenyewe, ndipo anapopata habari za Yesu kwamba Yesu huwapa haki na huwapumzisha walioshindwa na kuchoka kama yeye, ndipo hufurahi sana katika Yesu na kuingia kwenye pumziko la amani. Sehemu ambayo yale aliyoyaona zamani kuwa ni mzigo, sasa atayaona ni rahisi sana akiwa katika imani.

Paulo anahitimisha kwamba: “Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi.” (Gal. 3:25). WOTE walio wa kimwili wanapoamini hawawi tena kama zamani, bali huzaliwa upya na kuwa viumbe wapya. Sheria imewaongoza kwenda kwenye imani itendayo kazi za sheria kwa upendo, na ikishawafikisha inawaacha katika uongozi wa Roho: “ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yao wao, wasioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.” (Rum 8:4). Wanaoenenda katika uzao mpya wa Roho, hawawezi kuvunja sheria tena maana wao wenyewe wanakuwa kama sheria (Rum 2:14-16). “Kwa sababu dhambi haitawatawala ninyi mkiwa chini ya neema” (Rum 6:14).

SABATO KWENYE SHERIA.
_
Wajumapili wengi watakubaliana nami katika maelezo hayo juu, lakini inaporejea kwenye swala la sabato wanataka kukwepa na kusema kutunza sabato ni kuendelea kuwa chini ya sheria au ndiyo ufatafutaji wa haki kwa matendo ya sheria. Lakini nitaacha mtu ahukumu yeye mwenyewe kwa kulinganisha maelezo yaliyotolewa hapo juu, na kuona kama Je! Kutunza sheria ndiyo inamfanya mtu kuwa chini ya sheria na kutafuta haki kwa matendo au nini hasa? Ushahidi uliotolewa juu utamshawishi kila mtoto wa kweli wa Mungu.

Kuvunja sheria moja ni sawa na kuvunja zote (Yak. 2:10,11), hivyo kama unatunza 9 na kuvunja moja bado una hatia. Kama Wakristo waliomwamini Yesu na kutoka chini ya sheria na kuzaliwa upya na kuuongozwa kwa Roho, hatuishi kwa kufuata andiko kwamba usiguse, usionje, usishike, usivunje, n.k., (Kol. 2:20,21). Bali kwa kufuata sheria ya imani, na sisi wenyewe tumekuwa sheria yenyewe, tunatenda ya kwenye sheria kwa kupenda na kwa kutaka kwa namna ya roho, wala si kwa namna ya mwili ya usishike, uivunje, n.k. Sheria ya andiko imetuongoza kwenda kwenye imani ambako tunaongozwa na Roho, nayo inatuacha huru, kwa sababu kama tukiwa kwenye Roho basi hatuivunji sheria. Na ndiyo maana haituhusu, kwa kuwa yenyewe inawahusu wanaoivunja (1 Tim. 1:6-9).

masalianautume255.blogspot.com


Comments