Laana ya Sheria!
“…maana imeandikwa, Amelaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye.” Wagalatia 3:10
Hapa Paulo anaelezea laana aina mbili, laana kwa walio wa matendo ya sheria, na laana kwa wasioitenda sheria. Tuanze na upande wa wasioitenda sheria.
LAANA KWA WASIOTENDA SHERIA.
Danieli 9:11 “Naam, israeli wote wameihalifu sheria yako, kwa kugeuka upande wasisikize sauti yako; basi kwa hiyo laana imemwagwa juu yetu…kwa sababu tumemtenda dhambi.”
Laana inatupata pale tu tunapotenda dhambi, kwa kuiharifu sheria ya Mungu, na kutokusikiza maagizo yake. Watu wanapoiasi sheria, au kuibadilisha (kwa mfano badiliko la Sabato kutoka Jumamosi kwenda Jumapili), hapo ndipo laana inatokea, na hii ndiyo itasababisha kuangamizwa kwa ulimwengu huu. Dunia itaangamizwa kwa sababu watu wanaoikaa hawazitii sheria za Mungu, na hili halikuwatosha wakaamua hata kubadili amri yake, na hivyo wamelivunja agano walilokabiziwa na kuleta laana. Mungu anesema wazi wazi.
Isaya 24:4-6 “Tena dunia imetiwa unajisi kwa watu waikaao; kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele. Ndiyo sababu laana imeila dunia hii, na hao waikaao wameonekana kuwa na hatia, ndiyo sababu watu wanaoikaa dunia wameteketea, watu waliosalia wakawa wachache tu.”
Kwa hiyo laana imeila dunia kwa sababu watu wameziasi sheria na kuibadili amri. Na tunatakiwa kujua kabisa kwamba laana hutokea baada ya kushindwa kuitimiza sheria.
Kum. 27:26 “Na alaniwe asiyeyaweka imara maneno ya torati hii kwa kuyafanya. Na watu wote waseme, Amina.”
Kwa hiyo laana huja juu ya wasiotunza torati (sheria). Na torati yenyewe haikupita.
Mathayo 5:17 “Msidhani ya kuwa nalikuja kulitangua torati au manabii; la, sikuja kulitangua bali kulitimiliza.”
Matayo 5:18 “Kwa maana amini nawaambia, mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie.”
Luka 16:17 “…ni vyepesi zaidi mbingu na nchi vitoweke kuliko itanguke nukta moja ya torati.”
Kumb. 28:15 “Lakini itakuwa usipotaka kusikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake (pamoja na kutunza Sabato ya siku ya saba), nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata.”
Hivyo, ni hakika kuwa laana huja kama tusipotunza amri zote za Mungu. Na kinyume cha jambo hili pia ni hakika kwamba baraka huja kama tunatunza amri zote za Mungu.
Kumb. 28:1 “Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako.”
Kumb. 28:9 “BWANA atakuweka uwe taifa takatifu kwake, kama alivyokuapia; utakaposhika maagizo ya BWANA, Mungu wako, na kutembea katika njia zake.”
Kumb 11:26-28 Angalieni, nawawekea mbele yenu hivi leo baraka na laana; baraka ni hapo mtakapoyasikiza maagizo ya BWANA, Mungu wenu, niwaagizayo leo; na laana ni hapo msiposikiza maagizo ya BWANA, Mungu wenu, mkikengeuka katika njia niwaagizayo leo, kwa kuandama miungu mingine msiyoijua.”
Kwa hiyo kuna baraka kama ukitunza sheria, na laana kama ukivunja sheria. Sasa kama huu ndio ukweli wa Neno la Mungu, na kama tulivyoona umethibitishwa zaidi na Maandiko Matakatifu. Kwanini tena Mtume Paulo aseme kuwa “…wote walio wa matendo ya sheria wako chini ya laana…” Gal. 3:10?
LAANA KWA WALIO WA MATENDO YA SHERIA.
Tumegundua kwamba laana huja juu ya wale wasiotii sheria pekee, na kwamba baraka huja kwa wale wanaotii sheria yote. Kwanini tena Paulo aseme wote walio wa matendo ya sheria wako chini ya laana? Ni “kwa sababu wote wamefanya dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.” (Warumi 3:23). Na dhambi ni uasi wa sheria (1Yohana 3:4). Na mshahara wa dhambi ni mauti (Warumi 6:23). Hivyo kama wote wamefanya dhambi, wote pia wako chini ya laana na kustahili mauti, Kwa hiyo hata kama mtu akifanya matendo mema kiasi gani mbele za Mungu, matendo yake mema hayawezi kuiondoa laana aliyo nayo, hivyo mtu huyo hawezi kuhesabiwa haki kwa matendo anayofanya mpaka laana aliyonayo iondolewe kwanza.
Warumi 3:20 “Kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki kwa matendo ya sheria;…”
Lakini msifu Mungu kwamba mauti ambayo tungekufa sisi, Yeye alikufa kwa ajili yetu ili kupitia imani ya Yesu, ile laana na mauti tulivyovishindwa kuviondoa kwa matendo mema ya sheria, viondolewe na tusafishwe kabisa kwa damu yake iliyomwagika pale msalabani; maana, damu ya Yesu ndiyo inaweza kufuta laana na siyo matendo yetu.
Lawi 17:11 “…Nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi.”
Waebrania 9:22 “Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwagwa damu hakuna ondoleo.”
Marko 14:24 “Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi.”
Wagalatia 3:13 “Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, amelaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti.
Mtu hawezi kusafishwa kwa matendo mema ya sheria anayofanya, lakini anaweza kusafishwa na kuhesabiwa haki kupitia damu ya Yesu kwa kumwamini Mwana wa Mungu aliyetukomboa kutoka katika laana ya torati.
Warumi 3:23 “Kwa maana wote wamefanya dhambi…wanahesabiwa haki (au kuondolewa laana) bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumemweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa; apate kuonyesha haki yake wakati huu ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yeye amwaminiye Yesu.
Ku wapi, basi, kujisifu? Kumefungiwa nje. Kwa sheria ya namna gani? Kwa sheria ya matendo? La! Bali kwa sheria ya imani.”
Kwa hiyo mtu anaondolewa laana, na kuepushwa na mauti kupitia imani ya Yesu Kristo pekee, wala si kwa matendo mema anayofanya. Ni hakika kwamba mtu hawezi kujiondolea laana au kujifutia dhambi alizo nazo kwa njia ya matendo mema! Matendo mema hayawezi kuiondoa laana na kumfutia dhambi zake za nyuma. Basi kwa vile huu ndiyo ukweli uliothibitishwa na Biblia. Je wale waliohesabiwa haki kwa imani hawapaswi kutenda matendo mema? Au “Je twaibatilisha sheria kwa imani hiyo? Hasha! Kinyume cha hayo twaithibitisha sheria.” Warumi 3:31.
JE TWAIBATILISHA SHERIA KWA IMANI HIYO?
Katika sehemu mbili ziliyopita tumegundua kuwa wale wasioitenda sheria ya Mungu wako chini ya laana, lakini tumegundua pia kuwa wale wanaotaka kuhesabiwa haki kwa matendo mema ya sheria wanayofanya, na hawamwamini Yesu ili awaondolee laana na dhambi zao za nyuma, hawa nao wako chini ya laana ile ile. Kwa hiyo ni wale tu wanaomwamini Kristo na kutubu ili azifute laana na dhambi zao zote za nyuma, ndio hawako chini ya laana na wamehesabiwa haki bure kwa neema ya Mungu. Lakini Je wanapokuwa wamehesabiwa haki na kufutiwa laana yao hawatakiwi kutenda matendo ya sheria?
Wagalatia 2:17-18 “Lakini sisi wenyewe, kwa kutafuta kuhesabiwa haki katika Kristo, tulionekana kuwa wenye dhambi, Je! Kristo amekuwa mtumishi wa dhambi? Hasha! Maana nikiyajenga tena yale niliyoyabomoa, naonyesha yakuwa mimi mwenyewe ni mkosaji.”
Kwa hiyo kama mtu akivunja sheria anajenga upya laana ya Torati ambayo Kristo aliibomoa msalabani kwa ajili yake. na hivyo anajionyesha yeye mwenyewe kuwa ni mwenye dhambi; maana dhambi ni uvunjaji wa sheria, na mshahala wa dhambi ni mauti.
Hivyo wakati tunapokuwa tumehesabiwa haki na kufutiwa laana bure kwa njia ya imani pekee, ndipo tunapaswa kutenda matendo ya sheria ili kuepuka laana ya torati ijayo baada ya kushindwa kutunza sheria, kama tukiendelea katika dhambi huku tumehesabiwa haki, tutakuwa tunajenga laana ambayo Kristo aliivunja pale msalabani, na hivyo kustahili mauti maana mshahala wa dhambi (kuvunja sheria) ni mauti.
Lakini baada tu ya kuhesabiwa haki bure kwa njia ya imani, Je tupaswa kuishi vipi ili kuitimiza sheria na kuepuka laana yake tena?
Wagalatia 2:20 “Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.”
Kristo anakuwa ndani yetu kwa Roho Wake, Akituongoza kuipenda na kuitunza sheria yake, Aanaiandika barua au sheria yake rohoni mwetu.
Waebrania 10:16 “Hili ni Agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana, Nitatia sheria zangu mioyoni mwao, Na katika nia zao nitaziandika.”
2Wakorinto 3:3 “mnadhihirishwa kwamba mmekuwa barua (au sheria) ya Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama.”
1Petro 2:21-22 “…Kirsto naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake. Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake.”
Wafilipi 2:13 “Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.”
Waebrania 13:20-21 “Basi, Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu, awafanye ninyi kuwa wakamilifu katika kila tendo jema, mpate kuyafanya mapenzi yake; naye akifanya ndani yetu lipendezalo mbele zake, kwa Yesu Kristo; utukufu una Yeye milele na milele. Amina.”
Kwa hiyo mara tu tunapokuwa tumehesabiwa haki bure kwa njia ya imani, Mungu anafanya kazi ndani yetu kutusaidia kuitimiza sheria yote ili tuepuke laana na mauti.
Katika Biblia haki inahesabiwa katika hatua mbili, haki inayohesabiwa kwa njia ya imani, na haki inayohesabiwa kwa njia ya matendo.
Haki kwa njia ya imani
Hii ni haki inayohesabiwa bure kwa njia ya imani kwa wanadamu walioanguka na wadhambi, hauhitaji matendo mema yoyote ili kuhesabiwa haki hii, inatolewa bure kabisa kwa kila mtu anayeamini kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, na alikufa kwa ajili ya dhambi zetu ili atupatanishe na Mungu kwa kutuhesabia haki bure kwa njia ya imani. Hivyo haki hii ndiyo hutupatanisha sisi na Mungu, na kutufanya tuwe watenda kazi pamoja naye.
Warumi 3:22-25 “ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio…Kwa sababu wote wamefanya dhambi…wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika usitahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa; apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yeye amwaminiye Yesu.”
Haki kwa njia ya matendo.
Baada ya kuhesabiwa haki ya kwanza kwa njia ya imani, basi tumepatanishwa na Mungu, na tu watenda kazi pamoja naye, Kwa Mungu hakuna mapatano na uovu, kama tukiendelea kufanya dhambi, tunajitoa wenyewe kutoka upande wa Mungu na kujirudisha wenyewe chini ya laana, na hivyo tumemsulubisha tena Yesu mara ya pili ili atuondoe chini ya laana tena. Kwa hiyo wakati huu Mungu anatuhesabia haki kwa matendo tunayoyafanya kupitia uweza wake. Aidha tunaukubali uwezo wake utuwezeshao na Roho Wake atusaidiaye tusitende dhambi kwa kutokutenda dhambi kabisa, au tunazikataa nguvu zake zituwezeshazo na Roho Wake atusaidiaye tusitende dhambi kwa kutenda dhambi kabisa, na hivyo kuidharau neema yake na nguvu zake alizozitoa ili kutuokoa kutoka kwenye dhambi kabisa.
Kwa hiyo haki ya mara ya pili itahesabiwa kwa wale wanaoukubali uweza wa Mungu unaowasaidia kuzitii sheria zake, na umewawezesha kuzitii kikamilifu kabisa. Na laana na mauti vitakuwa ni mishahala ya wale wanaozikataa nguvu za Mungu zilizopo kwa ajili ya kuwawezesha wasifanye dhambi kabisa, na tayari wanaendelea katika dhambi kwa kuipinga nguvu ya Mungu na Roho Wake, wakiufuata mwili ambao huongoza kwenye uharibifu. Kama tutafanya unafiki kama huu, hatutahesabiwa haki ya mara ya pili, tutakuwa tumeidharau haki ya kwanza na kustahili mauti, na hatuwezi kuhesabiwa haki ya pili.
Warumi 2:11-13 “Kwa maana hakuna upendeleo kwa Mungu. Kwa kuwa wote waliokosa pasipo sheria watapotea pasipo sheria, na wote waliokosa, wenye sheria watahukumiwa kwa sheria. Kwa sababu sio wale wisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki.”
Hivyo, mara baada tu ya kuhesabiwa haki bure kwa njia ya imani katika Yesu, tunapaswa kuwa watendaji wa sheria, wala si wasikiaji tu.
“Semeni ninyi na kutenda kama watu watakao hukumiwa kwa sheria ya uhuru.” Yakobo 2:12
Kwa hiyo tuko chini ya laana kama hatutendi sheria, na chini ya baraka kama tunatenda sheria. Lakini matendo ya sheria bila imani na msaada wa Yesu, yameangushwa chini na imani izaayo matendo mema katika Kristo.
Mungu azidi kuwa Mwalimu wetu
Comments
Post a Comment