WARUMI 10:4 JE INATANGUA SHERIA??

Je! Warumi 10:4 inatangua Sheria??

SWALI: Warumi 10:4 inasema Kristo ni mwisho wa sheria ili tuhesabiwe haki kwa imani! Je hiyo inamaanisha nini? Je hatupaswi kutunza sheria tena?

JIBU: Warumi 10:4 inasema: “Kwa maana Kristo ni mwisho wa sheria, ili kila aaminiye ahesabiwe haki.”

Tatizo hapa sio kwamba Kristo ni mwisho wa Sheria, bali tatizo linalowasumbua wengi ni kujua kwa jinsi gani Kristo anakuwa mwisho wa sheria. Wakati mtu anapokuwa amemwamini Kristo kikamilifu, Kristo huchukua uongozi na kumtawala mtu huyo aliyeamini kiasi hicho kwa njia ya Roho Mtakatifu (Rum. 8:4,14), na mtu huyo hawezi kutenda dhambi kwa kuwa yeye amekufa, na uhai alio nao ni uhai wa Kristo aliye ndani yake (Gal 3:20; Rum. 6:1-11), Hawezi kutenda dhambi kwa kuwa tayari amemjua Yesu (angalia 1 Yoh. 3:6). Kitendo hicho ndicho huitwa haki ya Kristo, au haki ya Mungu; kwa sababu hali kama hiyo haimpati mtu kwa njia ya matendo mema anayojaribu kujitahidi kuyafanya, bali kwa njia ya kuamini tu; na ndiyo maana si haki ya mwanadamu bali ni haki ya Mungu; ambayo mtu yeyote anaweza kuipata kwa kuamini pekee.

Mtu yeyote aliyeamini kwa kiasi cha ukamilifu kama hicho, anasemwa kwamba amekufa pamoja na Kristo (Rum. 6:1-11), na unajua sheria humtawala mtu aliye hai na sio aliyekufa (Rum. 7:1). Mtu aliyekufa hawezi kuikosea sheria kwa kuwa amekufa wala hawezi kuhisi au kuwasha tamaa, hiyo ndiyo sababu wote walio na imani ya dhati ya Kristo na tayari wamebatizwa wanasemwa kwamba: “wameifia dhambi” (Rum. 6:2), na kwamba “dhambi haitawali maisha yao” (Rum. 6:6,12). Hivyo mtu yeyote ambaye amemwamini kweli Kristo, haongozwi na sheria, kwani sheria kwake imefika mwisho; hii ni kwa sababu yeye amekufa na sheria huwatawala na kuwaongoza walio hai na si wafu.

Mtu yeyote aliyekufa hawezi kuikosea sheria sehemu yoyote au upande wowote, na hivyo wote waliomwamini Kristo kwa imani ya ukamilifu namna hii hawaendi kinyume na sheria kwa sababu wamekufa. Hii ndiyo sababu Paulo angeweza tena kutuonyesha njia halali ya kuitumia sheria, kwamba “sheria haiwahusu watu wema wenye haki” (1 Tim. 1:8-9); yaan, haiwahusu wote waliomwamini Kristo. Bali “inawahusu wote wenye dhambi na waovu” (1 Tim. 1:9-10). Swali ni kwamba, Kwanini sheria isiwahusu wenye haki, lakini haiwahusu waovu? Ni kwa sababu wenye haki wamekufa na hivyo hawaikosei, lakini waovu au wenye dhambi ni wale wote ambao hawana Kristo na hawajafa bali wako hai, na kwa hakika sheria huwahusu walio hai ili ionyeshe wazi upuuzi wao jinsi ulivyo.

Je sheria hutungwa kwa ajili ya walio hai au waliokufa? Je Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inawatawala walio hai au waliokufa? Nadhani hakuna hata mtu mmoja tu anayeweza kuthubutu kusema Sheria za Nchi zinawahusu wafu! Vivyo hivyo, wote wanaomwamini Kristo na kufa pamoja naye, “hawako chini ya sheria”, “hawaongozwi na sheria”, “sheria kwao imefika mwisho”; kwa sababu wamekufa na sheria haiwahusu. Lakini ukweli unabaki pale pale kwamba wafu hawawezi kuikosea sheria, hivyo wanaomwamini Kristo na kufa naye, wanaitii sheria yote kikamilifu na kwa uhuru kana kwamba sheria haipo. Imani kama hiyo “huthibitisha sheria” (Rum. 3:21).

Hivyo, utaona kwamba wakati tunapomwamini Yesu na viungo vya miili yetu kufa, hapo ndipo sheria inafika mwisho, kwa sababu tumekufa; tumeifia sheria (Gal. 2:19). Na wakati huu ambao tumekufa, ndipo Kristo anatupa uhai wake ili uzima tulio nao usiwe wetu bali uzima wake ndani yetu, sisi tumekufa na hatuko hai tena, ila Kristo ndiye anaishi kwa ajili yetu: “Nimesurubiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.” (Gal. 2:20). TAFADHARI kumbuka kwamba kama tumekufa kweli, basi hatuvunji sheria yoyote; maana haiwezekani mtu aliyekufa kuwa na hatia au kosa lolote, hivyo 1. hatuongozwi na sheria, 2, hatuko chini ya sheria, 3, sheria imeisha au imefika mwisho, na 4, hatuzivunji sheria. Hizi ndizo sifa pekee za mtu aliyekufa katika Kristo kwa njia ya imani ya kweli, na hakuna uhitlafiano. Pia tunaweza kusema kwamba: “kwa hakika mimi nimekufa, na sina nguvu ya kuvunja au kutunza sheria; wala sheria hainihusu, ila uhai nilionao ni wa Kristo kwa njia ya imani, yeye ndiye anafanya kazi zake njema kupitia mimi”. Hii ndiyo HAKI YA KRISTO, ni kumwacha Kristo afanye mambo yake kupitia wewe, wakati huo wewe tayari umekufa wala huwezi kukosa. Ndiyo maana Paulo anasema yeyote aliye na wema huu au haki hii hawezi kujisifu maana hii sio haki kwa njia ya matendo bali ni kwa imani (Rum. 3:27).

Kwa hiyo: “Kristo ni mwisho wa sheria, ili tuhesabiwe haki kwa imani”. Yaani: “Kupitia Kristo tunakufa, tunaifia dhambi pamoja na sheria; na kwa njia hii sheria inafikia mwisho, haitutawali tena, na wala hatuivunji tena. Wafu hawavunji sheria na wala hawatawaliwi na sheria, wao wako huru kabisa kutoka kwenye sheria pia wako huru kabisa kutoka kwenye makosa.” Paulo anasema: “utu wenu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena; 7 kwa kuwa yeye aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi. 8 Lakini tukiwa tulikufa pamoja na Kristo, twaamini ya kuwa tutaishi pamoja naye;. . . 11 Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu.” (Rum. 6:6-11). Hata hivyo utu mpya au uhai tulionao kwa imani ya Kristo unapaswa kutii amri na sauti ya Mungu (soma Rum. 6:15-17), utu huo mpya tumepewa “ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi” (Rum. 8:4).

Wengi wanaotumia fungu hili ili kupinga sheria, ni wale ambao aidha wanapenda kufuata dhambi, au wanakataa kutunza sheria ya Sabato. Hata hivyo, wakati Adamu alipoumbwa, alikuwa mwenye haki bila kufanya matendo ya sheria yoyote yale, lakini katika hali yake ya haki, alipewa sheria ya kutokula tunda ambayo ilikuwa ni kama mhuri wa kuonyesha kwamba tayari Adamu ana haki, na kumpima kama atamtii Mungu au hapana! Na walipopuzia sauti ya Mungu wakala tunda, haki yao waliyokuwa wamehesabiwa bure ikageuka kuwa laana. Wakristo wote walio kwenye haki hii ya bure, kama wakipuuzia sauti ya Mungu wanajitoa wao wenyewe kutoka kwenye neema kwenda kwenye laana!

Walokole wengi watakubali kwamba Ibrahimu ni mtu mwenye haki kwa imani pekee kama ilivyo leo, na kwamba sisi sote tumeshauliwa kumuiga Ibrahimu. Kwa hakika huo ndio ukweli; Ibrahimu alihesabiwa haki bure kwa imani pekee bila kufanya tendo lolote jema (Rum. 4:1-3,9), lakini baadaye akapewa amri ya kutahiriwa na akaitii ili kumpendeza Mungu, na Paulo anasema amri hiyo ya kutahiliwa ilikuwa ni ishara ya kuonyesha kwa nje kwamba Ibrahimu kwa ndani tayari ana haki (Rum. 4:10-11). Vivyo hivyo Wakristo wote wanahesabiwa haki bure bila matendo mema yoyote, lakini wakishafanywa wenye haki, ndipo, ingawa miili yao imekufa, lakini kupitia uhai walio nao katika Kristo wanaitii sheria kama ishara ya kuonyesha kwamba tayari kwa ndani ni wenye haki. Wanaotii sheria kama vile na Ibrahimu alivyofanya baada ya kuhesabiwa haki, watapata haki (Rum. 6:16, 2:12-13), lakini wasiotii sheria kama vile Adamu na Hawa walivyofanya, watapata mauti (Rum. 6:16).

Kwa Neema ya Mungu share ujumbe huu angalau magroup 5 uliyonayo


                   0627729770

Comments