SHERIA ZILIZOFUTIKA

 ZIFAHAMU SHERIA ZILIZOFUTIKA NA SHERIA AMBAZO ZIPO MPAKA SASA. 


 Mpendwa msomaji nakukaribisha tena katika somo hili linalohusu makundi ya Sheria, wapi zilianzia na hata kutumika mpaka lini. Ikumbukwe kuwa katika Biblia yote kuna makundi manne ya Sheria kama ifuatavyo:-

 1. Sheria za Maadili ( Amri kumi) / Ten commandments. 

2. Sheria za Kafara na sikukuu. (The Religious Celemonial Laws) 3. Shera za  Vyakula. (Foods Laws) 4. Sheria za kiutawala ( The Civil Laws)  Ikumbukwe pia ktk makundi hayo manne, kuna Sheria zilizoandikwa na Mungu mwenyewe na kuna sheria ambazo ziliandikwa na Musa. Hii nitaielezea vizuri katika somo jingine hasa katika kufafanua andiko la Wakolosai 2:16,17. Kwa sasa tuangazie hasa makundi haya manne ya Sheria.

  1. Sheria za Maadili /Amri kumi ( The Ten Commandments/Decalogue)  Hizi ni Sheria ambazo ziliandikwa na Mungu mwenyewe  kwa Chanda cha kidole chake , Kumbukumbu la Torati 9:9-10, Kutoka 24:12 na zimeorodheshwa katika Kutoka 20:3-17 na Kumbukumbu la Torati 5:7-21. Amri kumi ni ufafanuzi wa Amri ya Mungu ya Upendo kama inavyotajwa katika Kumb. 6:5, Walawi 19:18 na Mathayo 22:37-40. 

Kwa hakika Amri ya 1 hadi ya 4 zinazungumzia Upendo wetu kwa Mungu, na Amri ya 5 hadi ya 10 zinazungumzia Upendo wetu kwa Jirani zetu. Hivyo utii wa Amri za Mungu ni kipimo ambacho kinaonesha upendo wetu kwa Mungu na kwa Upendo wetu kwa wenzetu.Yesu mwenyewe anathibitisha ktk Yohana 14:15 kwamba tukimpenda tutazishika Amri zake. Kumekua na dhana nyingi kwamba kwamba Amri kumi zilikuwepo ila Yesu aliziondoa jambo ambalo si la kweli, Kristo hakutangu hata kidogo Mathayo 5:17-19, bali alizipatia mkazo zaidi Mathayo 5:27,28. Amri kumi zitadumu milele, Zaburi 19:7, 119:89 ,111-112,142,144,152, Ktk mafungu haya limetumika neno “Shuhuda”, Je neno shuhuda  linamaanisha Amri kumi? Ndio!, soma Kutoka 25:16, 21-22 40:3,5, 17-21  31:18 34:28. 

Amri kumi ni shuhuda za milele  ziliandikwa na Mungu mwenyewe  ili tuongozwe kwazo hivyo mpaka leo zipo. Tunakiwa kuzitii kwani ni kipimo cha upendo wetu kwa Mungu Muumbaji wetu na jirani zetu. Kama unampenda Mungu hutaweza kuwa na miungu, wala sanamu n.k. Na kama unampenda Jirani hutomuibia, hutomshuhudia uongo, wala kutamani mali yake n.k. Ni Sheria hii ya Maadili ambayo ni NAKALA YA TABIA YA MUNGU YA UPENDO, na ya milele! Soma ulinganifu huu wa Mungu na Sheria yake:-   Rum 16:26 Mungu wa milele Zab. 111: 7,8 Sheria ni ya milele  Luk.18:19 Mungu ni mwema Rum. 7:12 Sheria ni njema  Yoh. 4:24 Mungu ni wa kiroho Rum.7:14 Sheria ni ya kiroho  Kumb. 32:4; Zab. 145:17  Mungu ni wa haki Rum. 7:12; Zab.119:172 Sheria ni ya haki  1 Yoh. 3:3 Mungu ni safi Zab. 19:8 Sheria ni safi


Mt. 5:48 Mungu ni mkamilifu Zab. 19:7 Sheria ni kamilifu  1Yoh. 4:8 Mungu ni pendo Rum. 13:10 Sheria ni pendo  1 Yoh. 1:5 Mungu ni nuru Mith. 6:23 Sheria ni nuru  Zab. 48:1 Mungu ni mkuu Hos. 8:12 Sheria ni kuu  Kumb. 32:4 Mungu ni Kweli Zab. 119:142 Sheria ni kweli  Isa. 5:16 Mungu ni mtakatifu Rum. 7:12 Sheria ni takatifu  2. SHERIA ZA KAFARA NA SIKUKUU.  (Religious Ceremonial Laws). Sheria hizi zimetajwa kwa uzuri ktk Mambo ya Walawi 1:1-17; 23-25 Sheria hizi zilihusiana na upatanisho na utakaso  wa dhambi. Ibada hizi zililenga katika mpango wa Mungu  wa wokovu, kafara zilizokuwa zikitolewa  ziliwakilisha kafara halisi ,yaani  Kafara ya Kristo.

  KAFARA WALIZOKUWA WAKIZITOA. A. Ngombe: Mambo ya Walawi  1:3-9 . B. Kondoo /Mbuzi: Mambo ya Walawi 1:10-13.  C. Njiwa /hua: Mambo ya Walawi 1:14-17 D. Sadaka ya Unga: Mambo ya Walawi 2:1-16.  Sheria hizo za sikukuu za kafara ziliambatana na baadhi ya sabato za maadhimisho , miandamo ya miezi, miaka, sadaka za vinywaji, sadaka za vyakula n.k, Soma Mambo ya Walawi 23:1-4, Hesabu 28:9 . Pia kulikuwa na sabato  ya mwaka wa  saba ilikuwa ikimwakilisha Kristo  kwani mwaka wa saba  ulikua ni mwaka wa kusamehe na kufuta madeni , kuonesha na kuwajali  na watumwa kuwaachia huru,  Soma mambo ya Walawi 25:6-7,  Sabato ya Mwaka wa saba Ilikuwa inamuwakilishwa Kristo atakayekuja kuwaachilia huru Wanadamu wote katika vifungo vya dhambi. Soma Luka 4:16-25. (Nitafafanua sabato hizi zilinavyotofautiana na ile iliyopo ktk Amri 10 ktk somo jingine). Mapumziko Haya kupitia kafara  yalielekeza kwenye pumziko ambalo mtu analoweza kupata kwa kumwamini Yesu . Sheria hizi zilikuwa ni kivuli zikimwakilisha Yesu  Ebrania 10:1-4  ,9:12-14, 23-26 10:19-22. Na kwasababu zilikuwa zikimuwakilisha Kristo Yesu mara alipokufa Msalabani Sheria hizi zilikoma /Ziligongomelewa Msalabani (Wakolosai 2:14-17, Efeso 2:14-16). Jambo la Msingi kulielewa na linawachanganya watu wengi ni kwamba Makusanyiko matakatifu ambayo pia yaliitwa Sabato ,ambayo yalianzishwa baada ya dhambi ili kumfundisha mwanadamu ili kumfundisha mwanadamu Mpango wa Wokovu , hayakuodoa sabato ya siku ya saba ambayo iliwekwa wakati wa uumbaji na kabla dhambi haijaingia (Mwanzo 2:1-3). 3. SHERIA ZA VYAKULA. (Food Laws) Sheria hizi zinapatikana katika Mambo ya Walawi 11 na pia Kumbukumbu la Torati 14. Sheria hizi zilihusu Vyakula , yaani vitu vinavyostahili kuliwa na ambavyo havistahili kuliwa .  Vitu vyote ambavyo maandiko yanasema kuwa ni najisi/vichafu hivyo si vyakula na vile vilivyotakaswa ndivyo  Vyakula alivyo ruhusiwa mwanadamu kula. Pamoja na kwamba leo watu wanakula  vitu najisi wakitoa madai kwamba


 Yesu alipokuja alivitakasa vyote lakini Biblia ipo wazi kabisa kuhusu swala hilo kwamba Damu ya Yesu ilimwagika msalabani  ili kututakasa WANADAMU wadhambi  na si kuwatakasa WANYAMA.  Hivyo madai ya kusema Yesu alivitakasa ni dhana ambayo inapoteza ukweli kuhusu kafara ya Yesu. Hata hivyo mtume Petro aliyekuwa na Yesu muda wote mpaka anapaa kurudi mbinguni, ASINGEKANUSHA neno la Yesu ktk njozi ya Matendo 10, nanukuu katika Matendo 10:14 “Lakini Petro akasema, Hasha, Bwana,kwa maana sijkula kamwe kitu kilicho kichafu au najisi”. Kama Petro angejua kuwa hizo najisi zimetakaswa ina maana tangu walipokuwa wakifanya utume wao baada ya Yesu kurudi mbinguni wangekuwa wanakula najisi zote!, nguruwe, sungura, paka, mbwa, nyoka, konokono n.k, lakini kwa kuwa Mwalimu wao asiyebadilika aliwafundisha na kuwaonesha mfano, waliishi kwa mfano huo na wala hawakufanya kinyume!. Sheria hizi za vyakula mpaka leo zipo kwani kusudi la Mungu tusitumie vitu vichafu kwani miili yetu ni hekalu lake (1 Kor 3:16,17; 6:19) na tumeonywa kwamba, “Basi mlapo au mnywapo, au mtendapo neno lolote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu (1 Kor 10:31). Ameahidi pia tutakapo zitii sheria hizi atatuepushia mbali magonjwa (Kutoka 15:26). Magonjwa mengi tunayoyaona na kuyasikia leo ni matokeo ya uvunjifu wa kanuni hii muhimu ya afya ya miili. 4. Sheria za kiutawala (The Civil laws).  Sheria hizi zilihusu Taifa la Israeli unaweza kuziona ktk Kutoka 21 na 22. Katika kipindi hicho Taifa hili  lilikuwa chini ya utawala wa Mungu  mwenyewe akiwa ndiye Mfalme wao,  Sheria hizi hazikuhusisha kabisa Wana wa Israel kujiokoa dhambini. Sheria hizi zilikoma pale Taifa la Israel walipodai kuwa wanataka kufanana na Mataifa mengine ambayo yalikuwa na Wafame wa kibinadamu  (1 Samweli  8:5-7), Hivyo wana wa Israeli kwa dai hilo WALIMKATAA Mungu na hatima yake  wana wa Israeli walianza kuchukuliwa  utumwani. HITIMISHO: Sheria zilizopo hadi sasa ni Sheria za Maadili (Amri 10) na Sheria ya Vyakula, lakini zile Sheria za Kafara (Zilikuwa kivuli cha ujio wa Yesu) zilikoma punde tu baada ya kifo cha Yesu msalabani na kukomesha makafara yote ya damu za Wanyama. Na zile za kitaifa (Taifa la Israeli wakati ule) hizi hazipo!. Zingatia pia kuwa Sheria za ndoa kibiblia pia zimo ktk Sheria ya Maadili (Maadili ya Ndoa ya Kikristo) hasa ktk zile 5 za mwisho zinazohusu upendo kwa jirani.  Wakati mwingine neno “Agano” hutumiwa vibaya kwa wengi kudhani Maandiko yote ya Agano la Kale/ Vitabu vya Musa na Manabii havina maana tena. Kumbe walipaswa kujua kuwa tunapozungumzia swala la Ukombozi wetu tunahusisha Maagano mawili tu; Agano la Damu za Wanyama na Agano la Damu ya Yesu Kristo. SIO HABARI YA VITABU VYA MUSA NA MANABII. Ushahidi wa jambo hilo umefafanuliwa vema katika kitabu cha Waebrania 8,9 na 10. Nitanukuu baadhi, Soma Waebrania 8:6,7  Waebrania 9:1-3; 9-15,19-22cf. Waebrania 10:1-9. Utaona Agano la kwanza lilikuwa la Damu za Wanyama na Agano la pili lilikuwa la Damu ya Yesu Kristo. Sasa Maandishi ya Agano la kale (Pentateuch na Hexateuch au vitabu vingine vya manabii) yanahusikaje hapo?. Utagundua ni makosa tu katika kushindwa kutofautisha au kutojua maana hasa ya “Agano” ktk muktadha wa vitabu (Agano la kale; Old Testament na Agano jipya; New Testament) au muktadha wa Ukombozi wa Mwanadamu (Agano la Damu za Wanyama; Old Covenant na Agano la Damu ya Yesu Kristo; New Covenant).  Aidha ifahamike wazi kwamba, HATUOKOLEWI KWA SHERIA HIZO, bali HUTUMIKA KAMA KIOO TU ILI KUTUELEKEZA KWA YESU TUNAPOJIKUTA KTK ANGUKO LOLOTE AU DHAMBI. Unapojitazama katika kioo na kugundua kuna uchafu usoni, kioo hakiwezi kukuondolea uchafu huo, kinakuonesha tu. Ndio maana Paulo anatwambia kuhusu kazi ya Sheria ktk Ukristo; Warumi 3:20b, Warumi 7:7. Kwa hakika Sheria hutusaidia kutambua dhambi ili tuitubu kwa Mungu, maana mtenda dhambi yeyote asiyetubu hataokoka. Shetani anatamani sana wanadamu watende dhambi na wasijue kuwa wametenda dhambi ili wasitubu na kusamehewa. Shetani anajua vema kuhusu Walawi 5:17. Kwa hiyo tusiihafifishe Sheria ya Mungu kwa kutumia kupindisha Maandiko ili yakubaliane na mafundisho ya madhehebu na kuacha maana ya Neno la Mungu. 


MUNGU ATUSAIDIE KUELEWA KWA JINA LA YESU KRISTO 

Comments

  1. Unazungumziaje swala la utuzaji wa sabato habari ya kupika,kuoga na n.k

    ReplyDelete
  2. Kwa Habari ya Kupika, kuoga siku ya Sabato hayo yalikuwa ni Mapokeo katika siku ya Sabato pia linae somo lake kuhusu hilo

    ReplyDelete
  3. https://masalianautume255.blogspot.com/2021/08/mapokeo-katika-siku-ya-sabato.html

    ReplyDelete

Post a Comment