NINI MAANA YA KUMWABUDU MUNGU KATIKA ROHO NA KWELI

 

Kumwabudu Mungu katika kweli: Roho Mtakatifu, kama alivyosema Yesu kwamba, “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.” Yohana 14:26. Roho Mtakatifu ndiye hutufundisha na kutuwezesha kukaa katika ukweli, na ndio maana anaitwa Roho wa kweli.

Yn 14:16-17 “Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; 17 ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.”

Mtu hawezi yeye mwenyewe kwa nguvu zake kumwabudu Mungu kwa kuifuata kweli. Ni lazima iwepo nguvu zaidi ambayo ni Roho ya Mungu itakayokaa ndani yake na kumwezesha kuitii kweli yote. Bila Roho Mtakatifu, mtu huwa hana bidii ya kumtafuta Mungu, huwa na chuki dhidi ya Mungu pale anapokutana na dhiki flani, huwa ni mwenye tamaa, huwa ni mwenye kila aina ya uovu.

Katika hali kama hiyo mtu hawezi kumwabudu Mungu katika kweli, wala hawezi kumpendeza Mungu hata kidogo, ingawa anaweza kujitahidi kwa kiasi flani na kujilazimisha kutii matakwa ya Mungu, lakini bado moyo wake unaichukia sheria ya Mungu, na kazi zote anazozifanya ili kutii matakwa ya Mungu, zinakuwa ni matendo ya kimwili tu, ambayo ni bure na hayampendezi Mungu, bali yanaongeza hasira kali ya Mungu juu yake. Hii ndiyo hali ya kutaka kuwa mwema mbele za Mungu kwa kuifanyia kazi sheria, kitu ambacho ni laana kwa mtu yeyote anayekifanya.

Lazima tujue kwamba “kumwabudu Mungu katika kweli”; hapa Yesu anamaanisha kumwabudu Mungu katika matakwa, au mapenzi yake yote; au kumwabudu kwa kuifuata haki yake yote ambayo ni sheria yake takatifu.

Kabla hatujaendelea zaidi kwanza tujue maana sahihi ya maneno haki, sheria, na kweli. Vinginevyo hakuna faida yoyote ya kujifunza somo hili.

“Haki” ni mambo yote yanayomfurahisha au yanayompendeza Mungu. “Sheria” ni njia ambayo Mungu anaitumia kuwajulisha watu haki yake, hivyo sheria ni maandishi, au maneno ambayo Mungu ameyaamuru yatekelezwe maana ndiyo yampendezayo au ndiyo haki yake. Wakati “Kweli” ni matokeo ya tendo lolote la haki ambalo tayari limekwishafanyika, hii ni kwa sababu ukweli hupatikana baada ya vipimo flani vya haki kufanyika. Kwa mfano: ukweli ni mafungu ya Maandiko yaliyokusanywa kwa pamoja ili kupata uwiano au balansi sahihi ya kitu kinacholengwa, na hiyo ni njia ya kupata kitu kwa njia ya haki, na kile kitu kinapopatikana ndio kinakuwa ni ukweli. Kwa kifupi ukweli ni tendo lolote la haki ambalo limehitimishwa, pia ukweli ni jambo lolote ambalo lipo, na liko sahihi.

Hivyo ukiangalia kwa makini utaona kuwa maneno, haki, sheria na kweli, hayatofautishwi katika maana moja kuu ambayo yote yanailenga, na maana hiyo ni kumpendeza Mungu au kufanya mambo ambayo Mungu anayapenda. Zaburi 119:151 inasema, “Ee Bwana. . .maagizo yako yote ni kweli” ikimaanisha sheria ya Mungu ndiyo kweli, lakini aya 172 inaongeza kwamba: “. . .Maagizo yako yote ni ya haki.” Hapa mwandishi anatambua kwamba sheria ndiyo kweli na haki ya Mungu, lakini katika aya 149 akaongeza tena kwamba: “Haki yako ni Haki ya milele, Na Sheria yako ni Kweli”. Haiwezi kusemwa wazi zaidi ya hapa, inaonekana wazi sana Biblia inayaunganisha maneno yote matatu kuwa kitu kimoja.

Lakini huu muungano uliopo unathibitisha kuwa sheria ni haki ya Mungu, na haki ya Mungu ni mambo yale yanayompendeza Mungu. Kuthibitisha zaidi Mungu Mwenyewe anasema: “Nisikilizeni, ninyi mjuao haki, watu ambao mioyoni mwenu mna sheria yangu; msiogope matukano ya watu, wala msifadhaike kwa sababu ya dhihaka zao.” Isaya 51:7. Inaonekana wazi kwamba Mungu Mwenyewe anafundisha kwamba sheria yake ndiyo haki yake, na katika aya 6 akasema: “mbingu zitatoweka kama moshi, na nchi itachakaa kama vazi, nao wakaao ndani yake watakufa kadhalika; bali wokovu wangu utakuwa wa milele, na haki yangu haitatanguka.” Hapa Mungu anauhusisha wokovu na haki yake, haiwezekani mtu yeyote kuokolewa kama anavunja sheria ya Mungu, na hii ndiyo sababu lazima sheria iwekwe kwenye moyo wa mtu, hii ni sawa na kusema kuwa Roho Takatifu ambayo huongoza kwenye kweli inawekwa ndani ya mioyo yetu, ili ituwezeshe kuitii kweli na kuwa wenye haki mbele za Mungu, hii ndio kumwabudu Mungu katika kweli na Roho; ni pale mtu anapokuwa na uwezo wa kutii maneno ya Mungu kwa kuwezeshwa na Roho Mtakatifu, na huo ndio wokovu.

Katika Isaya 51:6-7 Mungu ameonyesha kwamba sheria yake ndiyo haki yake, kisha akasema, “mbingu na nchi vitatoweka lakini haki yake haitatanguka”, haki yake ni tabia, au mapenzi yake ambayo ameyaagiza katika sheria yake. Hiyo haiwezi kutanguka, kwani kadri Mungu ambavyo hawezi kufa, ndivyo vivyo hivyo na tabia yake au mapenzi yake hayawezi kufa. Sheria au Torati ni maagizo ambayo Mungu amewaagiza wanadamu wayatimize na kwa kufanya hivyo wanafanya mapenzi yake au haki yake, Yesu alisema “mbingu na nchi zitaondoka lakini nukuta moja ya sheria haitaondoka” Mathayo 5:18, na kwamba “ni vyepesi zaidi mbingu na nchi vitoweke, kuliko itanguke nukta moja ya torati.” Luka 16:17. Hivyo haki ya Mungu ambayo mbingu na nchi zitatoweka lakini yenyewe haitatanguka ni sheria yake kama Yesu anavyoweka wazi.

Ngoja tuyageuze maneno haya matatu ili kupata maana nyingine zaidi na kisha tuhitimishe swali letu kwa ufafanuzi mwepesi na wa kweli.

Haki: kinyume chake ni “uasi” au “uharifu”, kila mtu atendaye mambo yasiyo haki atenda uasi, yaan, afanya mambo yasiyompendeza Mungu bali yanamchukiza Mungu. Sheria kinyume chake ni “kutokuwa na sheria” wote wasiomcha Mungu hawana sheria, hufanya mambo yanayowapendeza wao wenyewe, hutafuta haki zao wao wenyewe kwa akili zao na kujitumainia, haijalishi kama wanahuzuria kanisani au hawahuzurii kanisani, mfano wao ni Kaini aliyekuwa akisali kanisa moja na Habili, lakini Kaini hakuwa na sheria, wakati Habili alikuwa na sheria moyoni mwake na aliiti kwa njia ya imani. Wote wasio na sheria pia hawana imani.

Wakati mtu anapokuwa “hana sheria” anakuwa anafanya yanayompendeza yeye mwenyewe, anatafuta haki yake mwenyewe. Mungu alitoa sheria yake ili kwa kuifanya hiyo tufanye haki yake; yaan, kile kinachompendeza yeye. Mtu anapofanya kitu kinyume na mapenzi ya Mungu anafanya uasi na uasi ndiyo dhambi, na anakuwa anastahili mauti kama malipo au mshahara wake. 1 Yohana 3:4 (KJV) inasema: “Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi wa sheria.” Mtu anapoacha kutii sheria ya Mungu anafanya dhambi kwa kuwa dhambi ni tendo lolote ambalo si la haki, na lisilompendeza Mungu. Yesu aliposema kuna watu wengi wanaomwita Bwana, Bwana, lakini hawafanyi mapenzi ya Baba, alimaanisha wale wanaohuzulia ibada kama kawaida lakini hawatendi haki, yaan, hawafanyi yanayompendeza Mungu, na kwa kuwa wokovu unaendana na haki ya Mungu, hivyo inakuwa haiwezekani kwao kuokolewa siku ya mwisho kwa kuwa hawatii haki.

Yesu anapenda haki; yaan, anapenda kufanya mapenzi ya Mungu, na anachukia maasi; yaan, anachukia kila tendo la ukaidi linalofanywa kwa kupingana na sheria au maagizo ya Mungu, na hiyo ndiyo dhambi: “Umependa haki, umechukia maasi; Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekutia mafuta, Mafuta ya shangwe kupita wenzio.” Waebrania 1:9.

Ukweli: Kinyume chake ni “uongo”, uongo pia ni kila kitu ambacho si cha haki, au si halali. Kila kitu kisichompendeza Mungu hicho ni uongo, vivyo hivyo kila kitu kimpendezacho Mungu hicho ni ukweli. Haki ya Mungu ni Mapenzi ya Mungu au sheria yake, na huyo ndiyo kweli, wakati uongo ni matendo yote yasiyo ya haki, yasiyompendeza Mungu na hayatii sheria zake. Hivyo tunaona kuwa lengo kuu alilomaanisha Yesu wakati aliposema “waabudu halisi wamwabudu Mungu katika kweli”; alimaanisha wamwabudu kwa kufanya mapenzi yake yote, ambayo ni kutii sheria zake na kufanya haki yake; mambo ambayo yakishakufanyika, inakuwa imefanyika kweli.

Sasa turudi upande wa kumwabudu Mungu katika roho kisha tuhitimishe swali letu.

Kumwabudu Mungu katika Roho kama tulivyoona huko nyuma, ni kuwa Roho Mtakatifu katika maisha yetu. Mwanadamu yeye kama yeye hata kama akijilazimisha kiasi gani hawezi kutii amri yoyote ile ya Mungu kikamilifu, roho yake huwa na chuki dhidi ya sheria, naye mwenyewe matendo anayofanya ni ya kimwili tu ambayo Mungu hayahesabu kwamba yanastahili haki, hiyo ndiyo jinsi ya kutaka kuhesabiwa haki kwa njia ya sheria, ambayo ni laana kubwa kwa kuwa hakuna mtu yeyote aliye na hali kama hiyo anayeweza kuitii sheria yote kuanzia moyoni mwake, hivyo kazi zake zote anazofanya kwa nje katika mwili zinakuwa ni bure, na laana iko palepale na mauti na hasira ya Mungu ndio anazidi kuvistahili. Kadri anavyozidi kujitahidi na kujilazimisha kuitii sheria ndivyo anavyozidi kuichukia sheria kiasi kwamba anaona kama Mungu amemwekea mzigo usiobebeka, na laiti kama sheria ingekuwa haipo mbele zake, angekuwa anafanya hayohayo inayoyakataza ili kuuridhisha mwili wake. Katika hali kama hii mtu hawezi kuokolewa.

Kwa sababu hiyo, Mungu aliunda njia kwamba baada ya kumfutia mwanadamu dhambi zake zote za zamani kwa damu ya Mwanawe, angetuma Roho ije ndani ya mtu huyo anayemwamini Yesu ili imwezeshe na kumpa nguvu za kuushinda mwili wake pamoja na tamaa zake zote, Roho kwa kuongezeka huubadilisha kabisa moyo wa mtu na kuufanya upende kutii mapenzi ya Mungu, Roho inaleta bidii, nguvu, uwezo, ujasili, ili kushinda dhambi zote na kutii sheria zote za Mungu. Lakini Roho haiwezi kukaa kwa mtu ambaye hana imani, ili mtu aweze kuifikia hali hiyo, ni lazima kwanza awe na imani ya Kristo, jukumu kubwa tuliloachiwa sisi ni kuamini. Tunapaswa kuamini bila kusita kwamba Kristo alikufa kwa ajili yetu, ndipo tunapewa Roho, hasa baada ya kutubu na kubatizwa, itakayotupa uwezo wa kuishi bila kufanya dhambi katika maisha yetu.

Ndipo vita kati ya Roho na mwili inaanza. Roho inapigana na mwili na kulazimisha mwili utii sheria za Mungu, na mwili unapigana na Roho na kuilazimisha roho iutii mwili na tamaa zake, vita hii haiishi mapema kulingana na kama mtu anautii mwili au roho, lakini kama tukifuata roho, roho itapigana na mwili hadi mwili ufe kabisa usiwe unaleta tamaa za nje ili kufanya dhambi (soma Warumi 6). Fundisho hili la jinsi ya kuifuata roho, Paulo ameliandika katika Warumi 8 akasema kama tukiifuata roho hakuna laana tena kwetu, na tunakuwa na uwezo wa kuitii sheria ya Mungu.

Akasema: “hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.” (aya 1) yaan, juu ya wale ambao wamemwamini Yesu na wamepokea Roho Mtakatifu; Akaendelea kwamba: “Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti.” (aya 2); yaan, Sheria ya Roho ni sawa na sheria ya uhuru au ya kifalme kama Yakobo anavyoiita, sheria hiyo inaandikwa kwenye moyo wa mtu pale tu mtu anapopokea Roho Mtakatifu (angalia Waebrania 8:8,9; 10:16; na 2 Wakorinto 3:3), na anakuwa na uwezo wa kutii maagizo ya Mungu kwa kupenda na kujilazimisha. Wakati sheria ya dhambi ni pale mtu hana Roho Mtakatifu lakini anajaribu kujitahidi kutuza sheria, huyo hawezi kuitii torati na hivyo mauti ndiyo malipo yake.

Lakini watu waliomwamini Yesu na wamepokea Roho, na kwa sababu wanaifuata roho, wanakuwa na uwezo wa kutii torati na hivyo hakuna laana kwao, na siku ya mwisho wataokolewa. Paulo ameliandika jambo hili katika Warumi 8 na akasema wale wa sheria ya mauti ni wale wanaoufuata mwili na kujidanganya kwamba wanatii sheria ya Mungu, watu kama hao walikuwa Wayahudi, na tena watu kama hao ni watu wote leo ambao wanajilazimisha kutii sheria wakati roho zao zinaichukia tena hawana Roho Mtakatifu. Hao huufuata mwili nao huwaongoza kuitumainia sheria ingawa wanaichukia na hawaitimizi na hivyo laana haiondoki kwao na mauti ndio mshahara wao. Lakini Paulo anasema kwa sababu ya Yesu kuja na kuishi katika mwili kama wetu “aliihukumu dhambi katika mwili; 4 ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho.” (aya 3-4)

Kwa sababu Yesu alikuwa na asili mbili, moja ya kiungu na moja ya kibinaadamu, asili yake ya kibinadamu isingeweza kushinda dhambi wala kutii sheria za Mungu kama vile sisi katika asili zetu za kibinaadamu ambavyo hatuwezi. Hivyo Yesu akiwa kama mwanadamu kabisa kama sisi, alimtumainia Mungu ili amuokoe, na akapewa Roho Mtakatifu na akawezeshwa kuishi maisha yake yote bila kufanya dhambi hata moja. Kwa njia hii aliihukumu dhambi katika mwili ili na sisi kwa kumwamini yeye na kumtumainia yeye ili atuokoe, anatupa Roho Mtakatifu ili tuwe na asili mbili kama alivyokuwa yeye hapa duniani. Tunakuwa na Roho Mtakatifu ambayo ni asili ya kiungu inayokaa ndani yetu na kutuwezesha kuyatii maagizo ya torati kama Paulo alivyosema hapo juu, au kutuwezesha kuzikimbia tamaa za kimwili za ulimwengu huu kama Petro anavyothibitisha kwamba: “Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu (asili ya kiungu), mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa.” 2 Petro 1:4

Tumefanywa kuwa washiriki wa tabia ya kiungu, ambapo kwa kupokea Roho tunakuwa tumepewa asili ya kiungu ndani yetu ili tuokolewe na tamaa za ulimwengu huu na kuwezeshwa kuitii torati (Warumi 8:4). Bila kuwa na Roho hakuna mtu yoyote anayeweza kuishinda dhambi, na kujaribu kuishinda dhambi na kuitii sheria bila kuwa na Roho Mtakatifu ndani yetu, ni sawa na kuwa chini ya sheria, au kutafuta kuhesabiwa haki kwa matendo ya sheria, na kwa hakika hapo kuna laana na mauti pekee.

Lakini wakati tunapokuwa na Roho Mtakatifu, sio asili yetu ya kibinadamu inayofanya kazi kuitii sheria, bali ni asili ya kiungu ambayo imewekwa ndani yetu ndiyo inatuwezesha kuitii sheria na kufanya haki mbele za Mungu au kufanya mapenzi ya Mungu. Hapo sisi hatuna kazi yoyote tunayoifanya ili kutii sheria, bali kazi zote zinafanywa na Kristo aliye ndani yetu kwa Roho Yake. Ndiyo maana Paulo akaandika kwamba: “Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.” Wagalatia 2:20

Wakati tunapoamini tu, na Yesu akatupa Roho Mtakatifu, ndipo sisi hatufanyi kazi, bali Kristo ambaye anaishi ndani yetu kwa Roho yake ndiye anafanya kazi zote za sheria, wakati sisi kazi yetu ni kuamini tu na kumruhusu Kristo aingie ndani yetu ili atii sheria, hii ndiyo maana yeyote ambaye anauwezo wa kutii sheria asijisifu kana kwamba anafanya hivyo kwa matendo ya sheria, bali amshukuru na kumtukuza Kristo aliyeweka nguvu ya kiungu ndani yake kumwezesha kufanya hivyo. Wayahudi walimuuliza Yesu kwamba: “Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu?(yaan, matendo ya haki) 29 Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye.” Yohana 6:28,29. Kama Wayahudi wangemwamini Yesu wangepokea Roho ambayo ingewawezesha kufanya matendo ya haki kwa nje, lakini walisukumia mbali imani, na hivyo wakabaki na matendo yao wenyewe tu ya kimwili na ya kujilazimisha huku wakichukia sheria katika mioyo yao.

Lakini kutimiza sheria inamaanisha kuipenda na kuifanya kwa hiari bila kukwazika moyoni, na jambo hilo linawezekana tu kwa mtu ambaye anamwamini Yesu na amepokea Roho Mtakatifu, hii ndiyo HAKI YA KRISTO kama vile Yeremia alivyotabiri kwamba: “Katika siku zake [Yesu] Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu.” (23:5-6). Yesu ni haki yetu kwa sababu yeye ndiye anafanya matendo mema ndani yetu wakati sisi tunapomwamini. Jukumu letu ni kumwamini, kisha anatupa Roho ambayo ni asili ya kiungu itakayotusaidia kushinda dhambi, harafu ndipo tunapaswa sasa kuitii Roho na kuacha kufuata mambo ya kimwili, ndipo kama tukimwamini Yesu anatutunza katika nguvu zake ili tusianguke dhambini hadi siku atakayokuja kutuokoa: “Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.” 1 Petro 1:5.

Paulo alisema “wale waufuatao mwili hufikilia mambo ya kimwili ambayo ni dhambi, bali wale waifuatao roho hufikilia mambo ya roho ambayo ni haki” (Rum 8:5) pia “sheria yenyewe ni ya kiroho” (Rum 7:14), hivyo mtu ambaye ni wa kimwili hana Roho Mtakatifu anakuwa uadui na sheria ambayo ni ya kiroho wakati yeye ni wa kimwili (Rumi 8:7), Ndio maana Yesu alikufa msalabani ili kuleta amani kati yetu na sheria, maana alitaka kutupa Roho ili sisi na sheria tuwe wote wa kiroho, na hakuna uadui tena bali amani (Rumi 8:6) na kwa kuifuata Roho tunakuwa na uwezo wa kuitii sheria (Rumi 8:4, 8,9).

Hivyo ni muhimu ibada ya kweli iwe katika Roho na kweli, yaani katika Roho Mtakatifu na kufanya haki ya Mungu au mapenzi yake au sheria yake, ibada yoyote tofauti na hiyo ni uongo na kupotoka. Kwa sababu Roho ndiyo inamwendesha mtu kufanya mapenzi na haki ya Mungu ambayo ndiyo kweli. Na kwa hakika wokovu wote ndio umekalia hapo, kuwa na Roho ndani yetu itakayotuwezesha kumtii Mungu kikamilifu, bila hivyo mtu hawezi na kumwabudu Mungu; kwani huwa na chuki na vikwazo dhidi ya maagizo ya Mungu, na kama akipatwa na dhiki kidogo tu yuko tayari hata kumtukana Mungu.

MUNGU AKUBARIKI 

Kwa Msaada wa Kiroho piga 

0627729770 

0712336509 

Comments