NGAZI YA KUTUFIKISHA MBINGUNI

Ngazi ya kutufikisha Mbinguni

Posted Isack Mussa

Yesu alimwambia hivi nathanaeli: "Akamwambia, Amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.[Yoh1:51.].  Hapa Yesu alikuwa akimwambia nathanaeli kuwa Yeye ndiye ile ngazi aliyoiota yakobo.

Yakobo siku moja akiwa anamkimbia kaka yake Esau kwa sababu ya kuiba mbaraka wa uzaliwa wa kwanza ulifika usiku, akatafuta mahali pa kulala akatwaa jiwe moja  akaliegemea kama mto na kulala usingizi. Mara akiwa katika usingizi mzito aliota ndoto na tazama ngazi ndefu yenye mwangaza mwingi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni, na kisha akaona malaika wa Mungu wanapanda na kushuka juu yake. Juu ya ile ngazi alimwona Mungu akiwa amesimama; na kisha Mungu akamwambia kuwa Mimi ni Mungu wa ibrahimu, na Isaka Baba yako, Nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako, na pia Mungu akamwambia kwamba uzao wake utakuwa mwingi kama mavumbi ya nchi na kwamba Mungu atakuwa pamoja naye na kumlinda kila atakoenda  [Mwa28:11-15].

Kabla ya dhambi Adam na Eva walikuwa na upendeleo wa kuwasiliana na Mungu Ana kwa ana bila kuwa na pazia lolote kati yao. Lakini Baada ya Uasi Mahusiano na mawasiliano baina ya Mungu na Mwanadamu yalivunjika. Mungu na mwanadamu wakawa na uhasama Mkubwa na katikati yao pakawa na Ukuta Mkubwa. Mbingu ikawa mbali na Dunia na mwanadamu akatengwa mbali na uso wa Mungu. Mungu kukaa na mwanadamu ama mwanadamu kumfikia Mungu ikawa ni ndoto isiyowezekana kabisa. Lakini Yesu alikuja kuvunja Ukuta unaomtenganisha Mungu na Mwanadamu, na kurudisha tena mawasiliano baina ya Mungu na Mwanadamu. Mahusiano baina ya Mungu na Mwanadamu ambayo yalivunjwa kwa sababu ya dhambi yangerudishwa tu katika Kristo.

Yesu kabla hajaja duniani  alikuwa ni Mwana wa Mungu. Alikuwa katika Umbo la Mungu na kwa asili alikuwa Mungu. Mwana alikuwa ni Umoja na Baba wa Mbinguni, akitawala katika kiti cha enzi pamoja na Baba yake. Lakini Mwana hakufurahia fahari, Utukufu, na kutawala vitu vyote pamoja na Baba yake wakati mwanadamu yupo katika hali ya kupotea na kuangamia. Yesu aliamua kuacha utukufu na fahari ya Mbinguni, na kutwaa umbo la kibinadamu, akazaliwa kama mwanadamu.[Fil2:6-11].

Yesu akiwa kwa asili ni Mungu akatwaa Ubinadamu, na hivyo kuunganisha asili hizi mbili yaani Uungu na Ubinadamu kuwa mtu mmoja na mwanadamu mmoja Yesu kristo. Ile ngazi aliyoiota yakobo ilishuka na kuigusa nchi  na ncha yake nyingine  inazigusa Mbingu. Kwa kuunganisha Uungu na Ubinadamu ili kufanyika mwanadamu mmoja na mtu mmoja Yesu Kristo, Yesu Amezigusa Mbingu na kuigusa nchi pia. Yesu ameigusa Mbingu kwa upande wa Uungu wake, na kuigusa nchi kwa Upande wa Ubinadamu wake. Hivyo kwa kufanyika Mwili Yesu Ameiunganisha Mbingu na dunia kuwa kitu kimoja. Katika Yesu familia ya Mbinguni na familia ya duniani imekuwa moja bila kuteganishwa tena hata milele.

Baada ya Yesu kubatizwa na Yohana Mbingu zilifunguka, na sauti ikatoka Mbinguni ikisema; " Huyu ni Mwanangu mpendwa wangu ninayependezwa naye"[Math3:17]. Sauti ya Baba kwa Yesu kwamba Huyu ndiye Mwanangu Mpendwa, Ninayependezwa nawe, Inasema kwa niaba ya kila Mwanadamu. Katika Yesu familia ya Duniani imefanyika  Wana wa Mungu. Hakuna namna ambayo Mungu anaweza akamkubali Yesu kama Mwana wa Mungu bila kumkubali kama Mwana wa Adam, na kwa Kumkubali Yesu kama Mwana wa Adam ameikubali jamii yote ya wanadamu na kuwahesabu kuwa Wana wa Mungu kama anavyomkubali Mwanaye. Hakuna pia namna ambayo  Mungu anaweza akawakataa wana wote wa Adam bila kumkataa Yesu. Kama Mwanadamu, Yesu amejiungamanisha na jamii yote ya Adamu kwa kiungo kisichokatika kamwe, na kwa Uungu wake Yesu amejiungamanisha na Mungu pamoja na Mbingu yote. Umwilisho wa Yesu humpatanisha Mungu na Mwanadamu, na kumpatanisha Mwanadamu na Mungu.

Yesu ndiye ile ngazi aliyoiota Yakobo. Yesu ndiye njia ambayo kwayo Mungu huvusha Mkono wake na kumwokoa Binadamu. Yesu ndiye njia ambayo kwayo Mungu humbariki, humhudumia na kumlinda Mwanadamu. Yesu ndiye njia ambayo kwayo Mawasiliano yaliyokatika kwa muda mrefu baina ya Mbingu na dunia yanarudishwa. Ni kwa kupitia kwa Yesu ambapo Mungu aliwajia wanadamu na kukaa nao, na ni kwa kupitia kwa Yesu ambapo wanadamu wote watapandishwa juu mbinguni ili kuishi pamoja na Mungu, pamoja na malaika wa Mbinguni. Kwa kupitia Yesu tunalindwa na yule Mwovu. Kwa kupitia Yesu Malaika wanapanda na kushuka, Wakishuka na Mibaraka, Ulinzi, na Salamu toka kwa Mungu, na kuyapandisha maombi, shida, na mahitaji Yetu kwenda kwa Baba wa Mbinguni. Ni kupitia kwa Yesu kwamba Ahadi zote ambazo Mungu alimuahidia Ibrahimu zitatimia. Ni kwa Kupitia Yesu kwamba Wanadamu wote huokolewa na kufanywa wana wa Ibrahimu kwa imani, na kupewa Uzima wa milele, na kufanywa warithi wa Mbingu mpya na nchi mpya.

Mungu akubariki

Comments