KUWA CHINI YA SHERIA NA KUONGOZWA NA ROHO:
Bwana Asifiwe wana na binti za Mungu/; Natamani nikualike tutafakari maana ya haya maneno
1. Kuwa chini ya sheria
2. Kuongozwa na Roho
NINI MAANA YA KUWA CHINI YA SHERIA
Kuwa chini ya sheria inaweza ikawa na maana zaidi ya 1.
1. SHERIA,
Mfano katika Nchi Yetu ya Tanzania kuna Sheria inayokataza kumpa ujauzito mwanafunzi na Adhabu yake ni kifungo cha miaka 30. Sasa ikitokea mtu akifanya uovu huo mtu, huyu anakuwa Chini ya Sheria kwa sababu amevunja sheria ya Nchi. Hivyo hatakuwa huru kufanya mambo yake kwa uhuru kwa sababu sheria inamtaka afungwe miaka 30. Kwa hiyo maana ya kwanza ya kuwa chini ya sheria ni KUVUNJA SHERIA/ UTARATIBU/ KANUNI.
Mfano wa pili ikitokea mtu kaiba simu ya mtu na akakamatwa na Polisi, huyu mtu kwa vyovyote atakuwa chini ya sheria maana amevunja sheria inayokataza wizi na ndio maana wakati Fulani Polisi wakimkamata mharifu wanasema UPO CHINI YA ULINZI ina maana upo chini ya sheria au Dola. Kwa hiyo unapovunja sheria ina maana unakosa uhuru wa kufanya maamuzi yako binafsi zaidi ya kufuata sheria za mahali husika aidha mahakama, Gereza au Polisi.
2. Maana ya Pili ya kuwa chini ya sheria Ni KUONGOZWA NA SHERIA ili kutenda mema au uwe salama dhidi ya hatari. #Mfano ni huu. Wengi tunafahamu TAA ZA BARABARANI na MATRAFIC, ukifika kwenye mataa kuna Sheria inayokutaka au kukuongoza wewe Dereva KUSIMAMA au KUPITA kulingana na rangi ya taa inayowaka au kulingana na ruhusa ya Trafic. Ikiwa taa nyekundu imewashwa na wewe ukasimama hapo Umetii Sheria. Sasa endapo taa nyekundu imewashwa, lakini wewe ukapita tayari UMEVUNJA SHERIA.
Au #Mfano shuleni na katika vyuo lazima kuwe na sheria zinazo muongoza mwanafunzi kuwajibika sawasawa na utaraibu wa shule, na ikitokea mwanafunzi amevunja sheria moja wapo, basi atapata adhabu au kufukuzwa shule. Hivyo ili mwanafunzi awe na nidhamu ni pale atakapo tii sheria za shule au chuo, #Note hata maofisini kuna sheria. Hebu fikiria kwanza kama hakungekuwa na Sheria zinazowaongoza watu Kazini, shuleni, barabarani, bungeni, Nyumban nk, Hivi unadhani nini kingetokea? Bila shaka majibu unayo maana inawezekana hata wewe ni kiongozi mahali Fulani na unataka unaowaongoza wafuate sheria.
Zipo aina tatu za utii wa sheria.
1. Ni kutii sheria kwa woga. Yaani mtu anatii sheria kwa kuogopa jambo fulani baya: Mfano agano la kale kulikuwa na sheria inasema mtu akikutwa anazini apigwe mawe hadi kufa, ni kweli watu walikuwa wanatii, lakini kilichokuwa kinawafanya watii sheria ni kwa sababu ya kuogopa kupigwa mawe na sio upendo uliokuwa ndani yao, au mtu anatii sheria za Nchi kwa sababu anamuogopa Rais au kiongozi yeyote aliye juu yake, ina maana kama kiongozi hayupo wa kusimamamia utaratibu, basi mtu yupo ladhi kuvunja sheria.
Huku ni kushika sheria kimwili au Nidhamu ya woga. Aina hii ya Utii wa sheria ilitumiwa sana na Waisrael, na hata katika Serikali zetu.
2. Kutii sheria kwa Ushupavu: Wayahudi wengi walikuwa wanatii sheria kwa ushupavu ili waokolewe na waliamini kwamba ili mtu aweze kuokolewa ni lazima atii sheria za Tohara: Matendo ya Mitume 15:1 Wakashuka watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale ndugu ya kwamba, Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka.
Sheria ya Tohara ndio ulikuwa mgogoro mkubwa sana kati ya Paul na Wayahudi, 1 Wakorintho 7:18-19 Je! Mtu fulani ameitwa hali amekwisha kutahiriwa? Asijifanye kana kwamba hakutahiriwa. Mtu fulani ameitwa hali hajatahiriwa bado? Basi asitahiriwe. Kutahiriwa si kitu, na kutokutahiriwa si kitu bali kuzihifadhi amri za Mungu.
3. Ni kutii sheria kwa upendo/ bila shuruti wala woga. Aina hii ya utii wa sheria ni matokeo ya upendo ulioko ndani ya mtu baada ya kuokolewa yaani mtu anatii sheria sio ili akolewe bali anatii sheria kwa sababu ameshakwisha okolewa. Kwa mantiki hiyo kinachotangulia ni Upendo uliomo ndani ya mtu ndio unaleta msukumo wa utii wa sheria, ikiwa na maana kwamba ukimpenda Mungu huwezi ukavunja sheria kwa kuabudu miungu au kuchonga sanamu na ukimpenda mwenzako huwezi ukavunja sheria na ukamuibia wala kumshuhudia uongo,au huwezi ukamuua mwenzako, Yesu mwenyewe anasema #Yohana 14:15-17 Mkinipenda, mtazishika amri zangu.
1 Yohana 5:3"Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito.
Sasa Paulo anasema Katika #Wagaratia 5:16-18 Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria
Paulo amerudia rudia sana maneno
• #Kuenenda kwa Roho au Kuongozwa na Roho
• #Tamaa za mwili au Kuwa chini ya sheria
Sasa anayeongozwa na Roho ni yupi? Je, ni Yule Anayetii sheria au anayevunja sheria? Na aliye chini ya sheria ni yupi?
#Warumi 8:5-8 Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho.
#NOTE: kuna makundi mawili ya watu Paul anayabainisha:
1. Kundi la kwanza ni la watu wanaofuata mwili: Mfano mtu anaye Iba, anazini, anaua, anatamani, anavunja sabato, anabudu sanamu nk. Je, huyu mtu anaongozwa na Roho au au anaongozwa na mwili? Bila shaka anaongozwa na tama za mwili maana anavunja sheria za Mungu.
2. Kundi la pili ni la watu wanaoongozwa na Roho Mtakatifu: Mfano: mtu ambaye yeye hazini, haibi, haui, hatamani, havunji sabato, haabudu sanamu nk. Je, huyu mtu anaongozwa na mwili au anaongozwa na Roho Mtakatifu? Bila shaka atakuwa anaongozwa na Roho Mtakatifu maana anatii sheria za Mungu.
Na ndipo Paul anahitimisha kwa kusema hivi: Warumi 8:8,9 “”Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii #sheria ya #Mungu, wala haiwezi kuitii. Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.
#Kumbe mtu wa mwilini hawezi kutii sheria ya Mungu kwa sababu anatimiza tamaa za mwili, na kutimiza tamaa za mwili ni kuvunja sheria za Mungu.
#Mfano: Mtu akizini anakuwa amevunja sheria ya Mungu inayosema USIZINI, hapo ni kutimiza tama za mwili. Ina maana ukiongozwa na Roho huwezi ukavunja sheria ya Mungu kwa KUZINI.
Huwezi ukawa na miungu mingine
Huwezi ukaabudu sanamu
Huwezi kulitaja jina la Mungu bure
Huwezi ukavunja Sabato
Huwezi kuua,kuzini,kuiba , kusema uongo wala kutamani. Kwa sababu yupo Roho ndani yako anaye kuongoza kutii sheria za Mungu bila shuruti.
Kwa sababu torati/ sheria asli yake ni ya rohoni na sio ya mwilii, kwa hiyo mtu wa mwilini hawezi kutii sheria hata kidogo
#Kwa maana twajua ya kuwa torati asili yake ni ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi#. Warumi 7:14, Kwa hiyo ikiwa torati asili yake ni ya rohoni, basi hata wanao itii Torati ni lazima waongozwe na Roho Mtakatifu.
Kwa maana kazi ya Roho Mtakatifu ni kuwaongoza watu kutii sheria za Mungu na sio kuvunja
Ezekieli 36:27 Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.
Ukiona mtu anapinga sheria za Mungu jua ni mtu wa mwilini, na wala hana Roho Mtakatifu, maana Yesu mwenyewe anabainisha kwa kusema
Yohana 14:15-17 Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele;
ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.
Ahadi ya Yesu ni kwamba
1. Tumpende yeye.
2. Tushike amri
3. Ndipo tunapokea Roho mtakatifu.
Maana biblia inasema:
1 Yohana 5:3 Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito.
Mtu wa mwilini kutii amri anaona ni nzito kwa sababu ya tamaa za mwilini, lakini Roho akiwa ndani yako hakuna ugumu, maana biblia inasema Wafilipi 4:13
Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.
1 Yohana 2:3-4 Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake. Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake.
#Sasa ukiona mtu anasema amempokea Roho/ anaongozwa na roho wakati huohuo anapinga sheria, inabidi kuwa makini, na Biblia inasema: 1 Yohana 4:1 Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.
Sasa kuongozwa na Roho ni pale mtu anapotii sheria za Mungu kwa kuongozwa na Roho mtakatifu, na sio kwa nguvu zake mwenyewe au kwa hofu bali kwa upendo
Ukiongozwa na Roho matunda yake ni haya:
Wagalatia 5:22-24 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.
Anaposema # juu ya mambo kama hayo hakuna sheria# hana maana kwamba sheria haipo, Hapana bali hakuna sheria itakayokushtaki kwamba wewe ni mzinzi, au muongo nk..
Na mtu wa mwilini matokeo yake ni kuvunja Sheria za Mungu kila siku na haya ndio matunda yake.
Wagalatia 5:19-21 Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.
Mfano: mtu akiabudu sanamu anakuwa amevunja sheria ya Mungu inayosema Usijifanyie sanamu ya kuchonga.
#Mtu akiwa muasherati anakuwa amevunja sheria ya Mungu inayosema Usizini.
Hivyo kuongozwa na Roho sio kukataa sheria za Mungu, bali ni kutii sheria za Mungu, na kuwa chini ya sheria ni kuvunja sheria za Mungu, au kutii sheria za Mungu kwa Ushupavu.
Mungu Akubariki.
Comments
Post a Comment