Je Sabato ilibadilishwa?

Je Sabato ilibadilishwa?

Posted by Isack Mussa

Wengi husema kwamba baada ya kufufuka kwake Yesu, Wakristo hawakutunza Sabato ya siku ya saba ya wiki (Jumamosi). Lakini hudai kuwa kuanzia siku ya pentekoste walitunza siku ya kwanza ya wiki (Jumapili), kwa ajili ya kukumbuka ufufuo wa Yes. Je hii ni kweli? Je Mitume walibadilisha Sabato? Au Je baada ya Yesu kupaa mbinguni Mitume walifanya nini katika Sabato iliyofuata kabla ya Pentekoste?

Baada ya Yesu kupaa mbinguni wanafunzi wake walirudi Yerusalemu kutoka mlima wa mizeituni, vile vile kama Yesu alivyowaamuru kwamba wasitoke Yerusalemu mpaka atakapowaletea Msaidizi (Roho Mtakatifu). Hivyo sabato iliwakuta wamefika Yerusalemu.

“Kisha wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato.” Matendo 1:12

Walipofika Yerusalemu, yapata watu mia na ishirini walipanda orofani, walipokuwa wakikaa kina Petro kwa ajili ya kusali, siku hiyo ilikuwa ni siku ya sabato, na Biblia inasema.

“Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake.” Matendo 1:14

Katika siku hiyo hiyo ya sabato mtume Petro alisimama akahubiri Injili ya Yesu mbele ya wale watu 120 (angalia Mdo 1:15-20), tena sabato hiyo hiyo walipiga kura na kumchagua Mathiya mahali pa Yuda Iskariote (angalia Mdo 1:21-26). Lakini kesho yake, siku iliyofuata ndiyo ilikuwa Jumapili, siku ya Pentekoste, na Biblia inasema.

“Hata ilipotimia siku ya pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.” Matendo 2:1

Kwa hiyo mpaka hapo unaweza kuona kuwa japokuwa walihubiri neno la Mungu siku ya Pentekoste (Jumapili), lakini hawakuvunja sabato ya Jumamosi. Hivyo kila mchungaji anayetumia siku ya Pentekoste kudanganya watu kwamba sabato ilibadilishwa, ni muongo na anamfanya shetani kuwa baba yake kwa kusema uongo na kuwakosesha watu wa Mungu, wachungaji kama hao Yesu anawauliza.

“Mbona hamyafahamu hayo niyasemayo? Ni kwa sababu ninyi hamwezi kulisikia neno langu. Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika KWELI, kwa kuwa hamna hiyo KWELI ndani yake. Asemapo UONGO, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni MWONGO, na baba wa huo.” Yohana 8:43, 44.

Lakini wengine watasema, “hamna, sabato haikubadilishwa siku hizo, lakini ilikuja kubadilishwa na mtume Paulo badaye!”
Kwa hiyo tuangalie kama kweli Paulo alibadilisha sabato. Je ni kweli kwamba Paulo aliibadilisha sabato? Au yeye Paulo hakutunza sabato? Kwani desturi yake ilikuaje?

“Na Paulo kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimo, akahojiana nao kwa maneno ya maandiko sabato tatu.” Matendo 17:2

Wengine bado watasema, “hamna alikutana na Wayahudi pekee siku ya sabato, lakini Wayunani alikutana nao Jumapili.”
Je ni kweli kwamba Paulo hakukutana na watu wa mataifa siku ya sabato? Au Je alikutana nao siku ya Jumapili?

“(Paulo) Akatoa hoja zake katatika sinagogi kila sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wayunani.” Matendo 18:4

Wayahudi walipomshitaki Paulo, wakidai amevunja sheria. Je Paulo mwenyewe alisemaje? Aliposingiwa kuwa amevunja sheria Paulo Alisema.

“Ila neno hili naungama kwako ya kwamba kwa Njia ile ambayo waiita uzushi, ndivyo ninavyomwabudu Mungu wa baba zetu, nikiyaamini yote yanayopatana na torati na yaliyoandikwa katika vyuo vya manabii.” Matendo 24:14

Kwa hiyo Paulo aliiamini torati na manabii, na tofauti kati yake na Wayahudi ilikuwa ni imani ya Yesu, na siyo sheria au torati. Kwa hakika Paulo mwenyewe alipojitetea juu ya shitaka la kuvunja shelia alisema.

“…Mimi sikukosa neno juu ya sheria ya Wayahudi…sikuwakosa Wayahudi neno, kama wewe ujuavyo sana.” Matendo 25:8, 10

Hata walipomfikisha Rumi, Paulo aliendelea kusema wazi kuwa hajakosa katika sheria yoyote ile, alisema.

“…Ndugu zangu, ingawa sikufanya neno kinyume cha watu wetu wala neno lililopingamana na desturi za baba zetu, nalitiwa katika mikono ya Warumi, hali nimefungwa, tokea Yerusalemu.” Matendo 28:17

Hivyo, Paulo hakubadili sabato, wala sheria nyingine yeyote katika amri kumi, ila Wayahudi walimsingizia tu, kama vile watu wengi leo wanavyomsingizia kuwa alibadilisha sabato, lakini maneno yake yana nguvu kuliko maoni ya wapayukaji; maana yeye mwenye alisema, ”anaiamini torati na hivyo, hakukosa juu yake.”
Wengine hudai kuwa Yesu ndiye aliyebadili siku ya sabato kutoka Jumamosi hadi Jumapili, lakini hakuna ushahidi wowote wa jambo hilo, na kama Yesu alibadili sabato angeliwaagiza wanafunzi wake kutunza Jumapili! Lakini siyo hivyo, kwani mitume waliitunza sabato kama tulivyoona huko nyuma. Yesu mwenyewe alitunza sheria zote za Baba yake wala hakuonekana na kosa katika kutunza sheria, na kutunza sabato kwake ilikuwa ni desturi.

“Akaenda nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome.” Luka 4:16

Hivyo, Yesu hakubadili sabato bali aliitunza ili kutupa mfano kuwa nasi tunapaswa kuitunza sabato, ili kuonyesha utii wetu kwake na Baba yake. Kwa hakika, Yesu mwenyewe alithibisha kuwa sabato ni lazima itunzwe; maana haikupita na wala haitapita mpaka mwisho wa ulimwengu.

“Msidhani ya kuwa nalikuja kulitangua torati au manabii; la, sikuja kulitangua bali kulitimiliza.” Mathayo 5:17

“Kwa maana amini nawaambia, mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie.” Mathayo 5:18

“…ni vyepesi zaidi mbingu na nchi vitoweke kuliko itanguke nukta moja ya torati.” Luka 16:17

Hivyo, Yesu aliilinda torati kiasi kwamba haikupaswa hata nukta moja itolewe. Na kama mtu akitoa nukta moja kwenye torati, huyo atakuwa anampinga Yesu na Mungu, naye ndiye mpinga Kristo. Kwa hiyo kama Yesu, wala mitume hawakuibadilisha sabato ya siku ya saba.

JE NANI ALIIBADILISHA SABATO?

Katika Danieli 7:25, Mungu anaonyesha wazi kwamba kuna mamlaka itakayokuja kubadili sheria zake.

“Naye (mnyama) atanena maneno kinyume chake aliye juu…Naye ataadhimu kubadili majira na sheria…” Danieli 7:25

Je ni nani hapa duniani mwenye uwezo wa kubadili majira na sheria? Nani hudai kuwa anauwezo wa kubadili majira na sheria?

“Papa ana uwezo wa kubadili majira, kubadili sheria, na kuachana na mambo yote, hata maagizo ya Kristo.”
“Papa ana mamlaka na maranyingi ameyatumia, kuachana na amri ya Kristo.” –Decretal, de Tranlatic Episcop. Cop. (The Pope can modify divine law.) Ferraris’ Ecclesiastical Dictionary.

Kama mamlaka ya upapa katika kanisa la Romani Katoliki inao uwezo wa kubadilisha sheria ya Mungu. Je ilibadilisha Sabato takatifu ya Bwana? Je iliingiza utunzaji wa Jumapili badala ya utunzaji wa Jumamosi? Katika katekism ya mafundisho ya katoliki kuna maneno yafuatayo.

“Swali-Siku ya Sabato ni ipi?
Jibu-Jumamosi ni siku ya Sabato.
Swali-Kwanini tunatunza Jumapili badala ya Jumamosi?
Jibu-Tunatunza Jumapili badala ya Jumamosi kwa sababu kanisa la katoliki, katika balaza la Laodikia (364 B.K.), liliihamisha kutoka Jumamosi kwenda Jumapili.
Swali-Kwanini kanisa la katoliki liliweka Jumapili badala ya Jumamosi?
Jibu-Kanisa liliweka Jumapili badala ya Jumamosi, kwa sababu Kristo alifufuka kutoka kwa wafu Jumapili, na Roho Mtakatifu aliwashukia Mitume Jumapili.
Swali-Kwa mamlaka gani kanisa liliweka Jumapili badala ya Jumamosi?
Jibu-Kanisa liliweka Jumapili badala ya Jumamosi kwa ukamilifu wa ule uwezo wa Uungu ambao Yesu Kristo aliutoa kwake.” –The Convert Catechism of Catholic Doctrine, Peter Geiermann, C.SS.R., (1946), p 50

“Kanisa la Mungu limeona ni vema kuhamisha uazimishaji na utunzaji wa Sabato kwenda Jumapili!” –Catechism of the Council of Trent, p 402, toleo la pili (English), 1937 (kwanza ilichapishwa 1560)

“Kanisa Katoliki,” alisema kadinali Gibbons, “kwa wema wa kazi yake ya Uungu liliibadilisha siku kutoka Jumamosi kwenda Jumapili.” –Catholic Mirror Sept 23, 1983.

“Bila shaka kanisa la katoliki hudai kuwa badiliko, (la Sabato Jumamosi kwenda Jumapili) ilikuwa ni kitendo chake…na kitendo hicho ni ALAMA ya mamlaka yake katika mambo ya kidini.” –-H.F. Thomas, Chancellor of Cardinal Gibbons

“Jumapili ni ALAMA yetu ya mamlaka…kanisa liko juu ya Biblia, na uhamishaji huu wa utunzaji wa Sabato ni ushahidi wa jambo hilo la ukweli.” –Catholic Record of London, Ontario Sept 1, 1923.

Unadhani kwanini kanisa linadai liko juu zaidi ya Biblia? Kwa sababu kanisa limeibadilisha Sabato, na Wakristo wengi wanatii amri ya kanisa la katoliki kwa kutunza Jumapili, kuliko amri ya Mungu kutunza Jumamosi.

“…nithibitishie kutoka kwenye Biblia pekee kwamba ninalazimika kutunza Jumapili kitakatifu. Hakuna sheria kama hiyo kwenye Biblia. Ni sheria ya kanisa takatifu la katoliki pekee. Biblia inasema, ‘Ikumbuke siku ya Sabato na uitakase.’ Kanisa katoliki linasema, ‘Hapana, kwa nguvu zangu za uungu naitangua siku ya Sabato na kuwaamuru mtunze kitakatifu siku ya kwanza ya wiki. Na lo! ulimwengu wote uliostaarabika unainama chini katika utiifu wa hofu kwa amri ya kanisa takatifu la katoliki.” –kuhani Thomas Enright, Redemptorist Catholic College, kansans city, mo., lecture “sunday in history” p 56, February 18, 1884.

“Mamlaka ya kanisa yasingefungwa na mamlaka ya maandiko, kwa sababu kanisa limeibadilisha Sabato kwenda jumapili, siyo kwa amri ya Kristo, lakini kwa mamlaka yake lenyewe.” –Canon and Tradition, p 263

“Jumapili ni tasisi ya katoliki, na madai yake kuitunza, yanaweza kulindwa na misingi ya kikatoki pekee…kutoka mwanzo mpaka mwisho wa maandiko hakuna fungu hata moja linalothibitisha kuhamishwa kwa Ibaada ya hadhara ya wiki kutoka siku ya mwisho ya wiki kwenda ya kwanza.” –The Catholic Press, Sydney, Australia, August, 1900.

“Kanisa la katoliki kwa zaidi ya miaka elfu moja kabla hajawepo mprotestanti…liliibadilisha siku kutoka Jumamosi kwenda Jumapili.” –Catholic Mirror, September 23, 1893.

“Labda kitu kilicho wazi hasa, badiliko kuu la kimapinduzi kanisa lilifanya, lilitokea katika karne ya kwanza, Siku takatifu, Sabato, ilibadilishwa kutoka Jumamosi kwenda Jumapili. ‘Siku ya Bwana,’ ilichaguliwa, siyo kutoka katika agizo lolote lililoandikwa katika Maandiko, lakini kutoka katika ufahamu wa kanisa wa uwezo wake lenyewe…Watu ambao hudhani kwamba maandiko, yanatakiwa kuwa mamlaka yote, kimantiki huwa Waadventista Wasabato, na kutunza Jumamosi kitakatifu.” –(Saint Catherine Church Sentinel, Algonac, Michigan, May 21, 1995)

Kwa hiyo jumapili ni amri ya kanisa katoliki, na wote wanaoitunza jumapili wanatii mamlaka ya kanisa la katoliki, na siyo Biblia.

JE ILITOKEAJE………?

Miaka 2000 sasa karibu madhehebu yote na Wakristo wengi wanaabudu siku ya Jumapili! Je Sabato ilibadilishwa? Ndiyo! Na nani? Na Mitume au na Yesu? Hapana! Na nani sasa? Mungu alituonya kuwa mnyama angeazimu kubadili majira na sheria (angalia Danieli 7:25), hii kwa hakika, isingewahusu Mitume wala Yesu; kwa maana mnyama = taifa au ufalme (angalia Danieli 7:23). Mtume Paulo pia alituonya kuwa, siku ya Bwana isingekuja mpaka mtu wa kuasi, mwana mpotevu, mpinga Kristo afunuliwe. Yeye aketiye ndani ya kanisa la Mungu na kujiinua juu ya kila kiitwacho Mungu, akijifanya kana kwamba yeye ndiye Mungu (angalia 2Wathesalonike 2:3, 4, 7). Na kwamba uasi huu tayari ulikuwa kazini, na usingetokea mahali pengine bali humo humo kanisani (2Wathesalonike 2:7; Matendo 20:28-30). Haukupita mda mrefu baada ya siku za Paulo, uasi uliaanza kanisani.

Kama miaka 100 kabla ya Ukristo, Wamisiri walioabudu mungu mithras (mithraists) waliingiza sikuku ya jumapili, iliyowekwa kwa ajili ya kuabudu jua, na kadri Ukristo ulivyoongezeka, viongozi wa kanisa walitaka kuongeza hesabu ya washiriki kanisani. Ili kuifanya Injili iwe ya kuvutia kwa wasio-Wakristo, desturi za kipagani ziliingizwa kwenye sikukuu za kanisa. Siku ya kwanza ya wiki ikaanza kutambulika kama siku ya kupumzika ya dini na serikali. Mwishoni mwa karne ya pili, Wakristo wakaona kama ilikuwa ni dhambi kufanya kazi jumapili.

Mtawala wa dola la Rumi Constantine, aliyekuwa mwabudu jua, aliongoka kuwa Mkristo, lakini uongofu wake ulikuwa ni wa kisiasa zaidi na sio uongofu wa kubadilika moyo. Constantine alijiita mwenyewe askofu wa kanisa katoliki na alipitisha sheria ya kwanza ya nchi ya utunzaji wa jumapili katika mwaka wa 321 B.K. (angalia Schaff’s History of the Christian Church, vol. III chap. 75). Miaka minne badaye; yaani mwaka 325 B.K., Papa Sylvester akaita jumapili “siku ya Bwana,” na mwaka 338 B.K., Eusebius, askofu mfuasi wa Constantine, akaandika, “Mambo yote ambayo ilikuwa ni wajibu kuyafanya katika Sabato (siku ya saba ya wiki) sisi (Constantine, Eusebius, na maaskofu wengine) tumeyahamisha kwenda siku ya Bwana (siku ya kwanza ya wiki).” Badala kunyenyekea na kujitoa wenyewe kwa Bwana kama walivyokuwa mitume, viongozi wa kanisa walijiinua wenyewe na kujiweka mahali pa Mungu kana kwamba wao ndiyo Mungu. “…Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani.” 1Yohana 4:3.

Kwa hiyo utunzaji wa jumapili ni amri ya kanisa katoliki na kila anayeitunza anatii malaka ya kanisa katoliki, na kuvunja mamlaka ya Mungu (Sabato ya Jumamosi). Lakini madhebu na waKristo wengi wanatunza jumapili amri ya kanisa katoliki, Waprotestanti walioupinga mfumo wa ukatoliki na sheria zake, siku hizi wanatunza amri za upapa walioupinga zamani, wamemstaajabia mnyama (angalia Ufunuo 13:4). Hata kanisa katoliki lenyewe linashangaa jinsi gani waliokuwa wapinzani wake sasa wanaliinamia na kutii amri zake. Kwa hakika kanisa katoliki linachakusema juu ya Waprotestanti.

“Waprotestanti…hukubali Jumapili badala ya Jumamosi kama siku ya ibaada ya hadhara baada ya kanisa katoliki kufanya badiliko…kwa kutunza Jumapili, wanakubali mamlaka ya muongeaji wa kanisa, papa.” –Our Sunday Vistor, February 5, 1950.

“Ilikuwa ni kanisa Katoliki ambalo…lilihamisha pumziko hili (Jumamosi kama Sabato) kwenda Jumapili…Hivyo utunzaji wa Jumapili kwa Waprotestanti ni heshima kuu wanatoa, bila kujali wenyewe, kwa mamlaka ya kanisa (katoliki).” –Monsignor Louis Segar, “plain talk about Protestantism of today,” p 213.

“…Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani.” 1Yohana 4:3.

“Ni vizuri kuwakumbusha Wapresbyterian, Wabaptist, Wamethodist, na wote Wakristo wengine, kwamba Biblia haiwaungi mkono sehemu yoyote katika utunzaji wao wa Jumapili. Jumapili ni tasisi ya kanisa la Romani katoliki, na wale ambao huitunza siku hutunza amri ya kanisa katoliki.” –Priest Brandy, katika hotuba, iliyoripotiwa katika Elizabeth, N.J. “News” ya Machi 18, 1903.

“Swali: Je utathibitishaje kwamba kanisa lina uwezo kuamuru sikukuu na siku takatifu?
Jibu: Kwa kitendo cha kubadilisha Sabato kwenda Jumapili, ambacho Waprotestanti hukiruhuru; na hivyo kwa kupenda wanajipinga wao wenyewe, kwa kutunza jumapili kabisa, na kuvunja skukuu zingine nyingi zilizoamuriwa na kanisa hilo hilo.
Swali: Je utalithibitishaje hilo?
Jibu: Kwa sababu kwa kutunza jumapili, wanakubali uwezo wa kanisa wa kuweka sikukuu, na kuwaamuru chini ya dhambi; na kwa kutotunza pumziko [la sikukuu] lililoamuriwa na kanisa, wanakataa tena, kwa hakika, uwezo ule ule.” –Henry Tuberville, D.D.CR.C, (1833), in “Abridgment of the Christian Doctrine, p 58

“Swali: Je una njia nyingine yoyote kuthibitisha kwamba kanisa lina uwezo kuanzisha sikukuu za agizo?
Jibu: Lisingekuwa na uwezo kama huo, lisingefanya kile ambacho wanadini wa siku hizi wote wanakubaliana nalo, lisingeingiza utunzaji wa jumapili siku ya kwanza ya wiki, badala ya utunzaji wa Jumamosi siku ya saba, badiliko ambalo halina mamlaka ya Maandiko.” –Stephen Keenan (1851), katika “Doctrinal Catechism,” p 174

Kwa hiyo kama unatunza jumapili, unatii amri ya kanisa katoliki chini ya dhambi juu ya amri ya nne ya Mungu. Na dhambi ni uasi wa sheria za Mungu (angalia 1Yohana 3:4), hivyo kama mtu asipotii sheria zote au akivunja moja ya sheria za Mungu, huyo anafanya dhambi
(angalia Yakobo 2:10). Na malipo ya dhambi ni mauti (angalia Warumi 6:23, 5:12). Kwa hiyo kama tusipotunza Sabato [Jumamosi] tunafanya dhambi na kustahili kifo cha milele.

“Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafisi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki.” Warumi 6:16

Hivyo tunakuwa watumwa wake yule tunayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi (kumtumikia papa kwa kutunza jumapili) uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii (kumtumikia Mungu kwa kutunza amri zake zote) uletao haki. Kwa maana, “…ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki.” Warumi 2:13.

“Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu; BWANA ni mwenye fadhili na rehema.” Zaburi 111:4

BWANA ameweka siku kwa ajili ya kuyakumbuka matendo yake ya ajabu. Je unadhani ni kwa njinsi gani tuyakumbuke matendo yake ya ajabu?

“Ikumbuke siku ya Sabato uitakase…Maana kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.” Kut 20:8, 11. “Mungu akaibariki siku ya saba, akaitakasa.” Mwa 2:3 “…Yeye ameibariki, nami siwezi kulitangua.” Hes 23:20 “…Wewe Bwana, umebariki nayo imebarikiwa milele.” 1Nya 17:27

“Kwa maana ameinena siku ya saba mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote;…“Basi imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu. Kwa maana yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi zake.” Waebrania 4:9, 10

Mungu atujalie tuitunze Sabato sheria yake, na siyo jumapili sheria ya mwanadamu, “…Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.” Matendo 5:29.

Comments